Ni Muhimu Makonda Amalize Utata Huu..!!!


Wakati Rais John Magufuli alipoteua wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri kuliibuka maneno mengi, hasa mitandaoni kuwa mmoja wa watu walioteuliwa hana elimu ya kutosha kustahimili kazi hiyo.

Maneno hayo yalifikia hatua ya watu kusema kuwa mtu huyo amesomea masuala ya hoteli. Ilikuwa bahati kwamba walioteuliwa wakati huo walitakiwa wahakikiwe elimu yao kabla ya kuapishwa.

Kabla ya kula kiapo cha maadili ya uongozi, Rais Magufuli alizungumzia suala hilo na baadaye kumtaka mtu aliyetuhumiwa kuwa hana elimu ya kutosha, aonyeshe hadharani cheti chake na alifanya hivyo.

Huo ulikuwa mwisho wa maneno dhidi ya mteule huyo.

Rais Magufuli alilimaliza suala hilo kirahisi kwa kuwa elimu si kitu cha kuficha kutokana na ukweli kuwa mtu hupata elimu hadharani na huwa pamoja na watu wengine wengi, kama walimu na wanafunzi wenzake ambao huwa kama mashuhuda kuwa alipata elimu na kumaliza kama ilivyotakiwa.

Hivi sasa kuna maneno mengi kwenye vyombo vya habari hasa mitandaoni kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni utata wa elimu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Mengi yameshaandikwa dhidi yake kuhusu elimu yake na hata tuhuma kuhusu jina analotumia kuwa si lake. Tunajua kuwa Makonda ana haki ya kujibu au kutojibu tuhuma hizo kutokana na ukweli kwamba kwanza ni faragha yake, na pili kama alisoma inajulikana dhahiri na kama hakusoma hawezi kuficha hilo kwa kuwa litajulikana tu.

Lakini, Makonda ni kiongozi wa umma ambaye hatakiwi kuwa na tuhuma zinazoweza kufanya watu anaowaongoza wapoteze imani naye.

Ni kweli yamesemwa mengi dhidi yake na ambayo hatungependa ajitokeze kuyazungumzia. Lakini hili la elimu liko wazi na ni jepesi kulijibu kuliko mengine mengi ambayo hata akitoa majibu sahihi vipi, bado yataacha maswali.

Isitoshe, suala la elimu halina uhusiano na wadhifa wake kwa kuwa Rais hutumia vigezo tofauti kuteua wakuu wa mikoa. Kwa hiyo, awe na elimu au asiwe na elimu, ukuu wa mkoa uko palepale.

Lakini, kwa kuwa suala lake la elimu linazungumzwa kwa jinsi ambayo inatia shaka, basi Makonda hana budi kujitokeza na kuweka hadharani elimu yake ili liishe na kuruhusu mambo mengine yaendelee.

Ni kweli kwamba inawezekana suala hilo limeanzishwa kwa sababu amegusa watu katika kampeni aliyoianzisha ya kupambana na watumiaji na wafanyabiashara ya dawa za kulevya, lakini hilo haliwezi kumfanya apuuzie tuhuma zinazohusu utata wa elimu yake.

Kuweka bayana suala la utata wa elimu yake, kutawanyamazisha hao waliomteua na zaidi kutawafanya wananchi watambue kuwa kumbe maneno yote hayo yanatokana na kugusa watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Pia, kama mteule wa Rais, ni lazima Makonda aiondolee mzigo mamlaka iliyomteua kwa kuondoa utata huo. Wakati Rais alipokuwa anazungumzia maneno ya watu dhidi ya mteule wa nafasi ya ukurugenzi wa wilaya, aliweka bayana kuwa hao wanaosema hayo wanadhani ofisi yake haifanyi uchunguzi wa kutosha kabla ya kutangaza wateule.

Kuthibitisha kuwa ofisi yake ilifanya uchunguzi, alimtaka aonyeshe cheti chake juu na kuita wapiga picha wachukue tukio hilo. Rais aliona umuhimu huo kwa kuwa alijua tuhuma hizo zilikuwa zikielekea kuionyesha kuwa ofisi yake haifanyi tathmini ya kutosha kabla ya kuteua.

Hatudhani kama Rais atakuwa akifanya kazi hii kwa kila mteule wake. Kwa hiyo, ni vizuri kwa Makonda kuchukua jukumu hilo na kuiondolea mzigo mamlaka iliyomteua.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. HANA BUDI, VYETI MEZANI KWANZA ALAFU ABAKIE NA DAR-ES-SALAAM YAKE

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad