Nilivyomdhania Magufuli Kumbe Sivyo...


Na. M. M. Mwanakijiji

Kwa baadhi yetu tuliokataa kuvingirisha mikono yetu kuunga mkono mabadiliko yaliyobinafsishwa kwa mtu mmoja tulijikuta hatuna budi kumuunga mkono Magufuli tukiamini anawakilisha mabadiliko ya kweli. Binafsi niliamini kabisa kuwa Taifa lilikuwa linamhitaji kiongozi kama Magufuli kuweza kulinasua mahali lilipo kuliko kiongozi yule mwingine toka upinzani. Niliamini kabisa kuwa Magufuli akishika madaraka atakuwa na kazi kubwa ya kulirejesha Taifa katika misingi yake ambayo inaonekana ilikuwa imepotea.

Hatua zake mbalimbali za mwanzo kushughulika na kubana matumizi, kupambana na ufisadi na kuondoa watendaji mizigo a.k.a majipu kulinifanya niamini kabisa kuwa Magufuli kazi aliyonayo akiendelea na kasi hiyo basi ndani ya miezi sita tu atakuwa ameleta heshima katika utumishi wa umma, kurejesha heshima kwa Watanzania na fahari ya taifa letu kurudishwa. Niliamini kabisa kuwa Magufuli atafanya kazi hii bila woga, huruma, husuda, wivu, au kusita sita. Kwamba, hatomwangalia yeyote, popote na kwa lolote. Ndani ya miezi sita hivi na kabla ya ujio wa bajeti ya kwanza ya serikali yake basi Magufuli atakuwa ameshaweka alama za namna gani taifa linataka kwenda na kila kiongozi atakuwa amepata ujumbe.

Nilifanya makosa.

Nilifanya makosa kwa sababu nilidhani hii ni kazi rahisi kwa Rais. Nilidhani ni kazi ya kutimua huyu, kuondoa yule na kumleta yule mwingine. Nilidhani ni kazi ambayo akimaliza teuzi mbalimbali basi atakuwa ameipanga serikali yake kwa ajili ya kuchapa kazi.

Sasa najua kuwa uamuzi wake wa kushughulika na watu kwanza kabla ya mfumo ni jambo muhimu sana. Ulikuwa ni uamuzi sahihi na unajitahi kutetewa. Watu ndio hutengeneza mfumo; ni watu ndio ambao hukaa chini na kufanya maamuzi mbalimbali yenye kuathiri (kwa uzuri au ubaya) uwepo na utendaji wa mfumo wa utawala. Ukiwa na watu wabovu, wabinafsi na wenye mwelekeo wa ufisadi basi mfumo utakuwa mbovu, wa kibinafsi na wenye uelekeo wa kifisadi kwa sababu moja kubwa; wale wenye kuiwamba ngoma ngozi huivutia kwao! Mfumo wetu wa utawala wa kifisadi ulitengenezwa na watawala wenye mwelekeo wa kifisadi. Matobo (siyo matundu) kwenye sheria zetu vilitengenezwa na watu ambao walijua wakiziba na wao watakuwa wamejizibia.

Magufuli asingeweza kutengeneza mfumo mwingine kwa kutumia watu wale wale walioutengeneza mfumo huu wa sasa na hasa kama watu hao ni wanufaika wa mfumo huu. Ingelikuwa ni sawa sawa na kumtaka Rais awalazimishe watu wakate matawi ambayo wamekalia huku wakijua kwa kufanya hivyo wataangukia mtoni kwenye mamba wengi. Hakukuwa na jinsi nab ado hakuna jinsi ni lazima kuwaondoa hawa na kuwashughulikia ili kuleta watu wenye fikra zinazoakisi mwelekeo wa serikali yake.

Ni kwa sababu hiyo, kumbe kazi ile ya miezi sita kwa kweli haiwezekani. Ni kazi ambayo inapaswa kuwa endelevu na yenye matokeo bora. Tayari tumeanza kuona dalili za yaliyomo ndani ya ripot ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) na tayari inatisha kama ilivyotisha mwaka 2006 na miaka iliyofuatia. 

Kwa muda mrefu tumekuwa tukijulishwa juu ya uchafu wa watendaji wetu na taasisi zetu na mara karibu hizo zote tumekuwa tukionesha kushtushwa na kusikitishwa tukiamini kuwa labda mwaka unaofuatia mambo yatakua tofauti. CAG aliyepita alikuwa anarudia baadhi ya hoja mwaka baada ya mwaka na wakati mwingine kuhusiana na taasisi au watu wale wale. Na safari hii tusije kushangaa kuwa hata CAG wa sasa anaweza kujikuta amegusa maeneo yale yale; matumizi mabaya ya sheria ya manunuzi ya umma, fedha kutumiwa bila maelezo, kutopatikana kwa vitabu vya masuala ya fedha wakati wa ukaguzi, na upotevu wa fedha za umma kwa namna ambayo inadokeza tu kuwa zimeliwa.

Magufuli basi ana kazi kubwa; kushughulikia viongozi wabadhirifu, wazembe, wezi, na wenye kutumia madaraka yao vibaya na wakati huo huo kupanga na kusimamia serikali yake huku akiuunda upya mfumo uliojaribiwa na kuharibiwa.

Kwa mwendo alioanza nao hakuna shaka yoyote jambo moja lilikuwa sahihi kwa upande wangu; kuunga mkono mabadiliko haya. Wapo wanadhani hali ni ngumu sasa na kuwa serikali inabana naamini bado hatujaona hasa ugumu kwani hadi hivi sasa bado serikali inahangaika na madudu ya nyuma na yanatisha. Kusahihisha uchumi (correcting an economy) ambao umejengwa na kusimamiwa na utamaduni wa kifisadi (corrupt culture) haiwezekani kuwa ni jambo moja.

Ni kwa sababu hiyo naamini:

1. Kuanza kazi kwa mahakama za kushughulikia ufisadi na uhujumu uchumi kunahitajika mara moja

2. Sheria ya CAG ifanyiwe mabadiliko mapema zaidi ili CAG awe na madaraka ya kutoa agizo la kusimamishwa kazi na hata kufikishwa mahakamani kwa mtendaji yeyote wa umma ambaye uchunguzi wake (CAG) unaonesha kuwa kuna uvunjaji wa sheria. Ikiwezekana ofisi ya CAG iwe na Waendesha mashtaka wake kama ilivyo kwa TAKUKURU. Haipaswi madudu yam waka mzima yanasubiri mwaka mwingine kujulikana. CAG anapofanya ukaguzi na kukuta madudu na ushahidi wa kisayansi upo (forensic evidence) basi hatua zichukuliwe mara moja. Siyo awe na uwezo wa kupeleka mashtaka lakini kwa kupendekeza kwa DPP au hata yeye mwenyewe washutumiwa watiwe mbaroni, mali zao zinazohusiwa kupatikana kwa njia haramu kukamatwa ili zije kufilisiwa wakikutwa na hatia.

3. Sheria ya Usalama wa Taifa inahitaji kufanyiwa marekebisho ya haraka – hili ni jambo ambalo limekuwa katika mada zangu kwa karibu miaka kumi sasa. TISS bado ni dhaifu sana na udhaifu wake umechangia sana kutamalaki kwa utamaduni wa kifisadi. Natumaini Magufuli hatochukua muda mrefu kuifumua hii taasisi kwani ndio moyo wa taifa. Ikilegea taifa liko mashakani.

Kuna na mengine mengi ambayo naamini Magufuli atayafanya kwani tayari ameshaanza kuyafanya na kuwa endapo atafanikiwa tutakapofika mwisho wa mwaka huu kama taifa tutashusha pumzi kidogo kwani angalau tutakuwa katika mazingira ya kusema “kweli hakika huyu alikuwa anahitajika”.

Ni wazi pia kutokana na kazi hii ngumu ambayo tunaamini Magufuli anaiweza kutakuwepo na wasema “hapana” na waleta “vikwazo”. Wale ambao wataona maslahi yao yanaguswa na kuwa pale walipokuwa wakihemea sasa panaanza kuondolewa. Watakuwepo watu ambao watajaribu kudhulumu na kuharibu jitihada hizi; raia wa kawaida, watendaji serikalini, wabunge na tusije kushangaa hata watu wake wa karibu. La maana ni kukaza mwenzo na kuendelea kusafisha serikali, kuleta uwajibikani, na nidhamu ili hatimaye Ujenzi Mpya (Reconstruction) wa taifa letu uanze tena kwani pale tulipoacha kulijenga tulianza kulibomoa. Hizi ni Zama Mpya, zama za ujenzi mpya wa taifa letu.

Katika hili, naamini nilikuwa sahihi na bado naendelea kuwa sahihi. Magufuli ni kiongozi wa zama hizi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad