Siku chache baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Harrison Mwakyembe kutishia kukifuta Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kwa madai kuwa kimesahau misingi yake ya kazi na kuanza kujishughulisha na siasa, kesi ya kupinga uchaguzi wa chama hicho imefunguliwa.
Kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma ambapo mlalamikaji ni Godfrey Sabato John Wasonga dhidi ya TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wasonga anaitaka mahakama ihairishe uchaguzi wa TLS hadi hapo Bunge litakapokutana mapema mwezi ujao kuweza kubadili kanuni zinazoongoza chama hicho.
Kwa taarifa za wadau kutoka kwenye mitandao ya kijamii zinadai kuwa hii ni njama ya Waziri Mwakyembe kumkwamisha Tundu Lissu kugombea urais wa TLS.
Waziri Mwakyembe hivi karibuni amenukuliwa akisema kuwa tatizo kubwa ni mtu mwenye kofia ya uongozi kwenye chama cha kisiasa kugombea urais wa TLS. Miongoni mwa wagombea ni Tundu Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA ambapo tayari ana kofia ya uongozi kwenye chama cha siasa.
Aidha, inadaiwa kuwa, mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa na Bunge kuhusu TLS ni kuzuia kiongozi wa chama cha siasa kuwania urais wa TLS.
Source: Swahilitimes