WAKATI Yanga ikishuka Uwanja wa Taifa leo kuivaa Ruvu Shooting ya Pwani katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, beki wa kati wa kimataifa Togo, Vincent Bossou, amesema yuko tayari kuondoka katika klabu hiyo, lakini baada ya kulipwa malimbikizo ya mishahara yake ya miezi minne anayoidai klabu hiyo.
Bossou aliandika madai yake jana katika akaunti yake ya Instagram na kukanusha taarifa kuwa anadai mshahara wa mwezi mmoja tu wa Januari kama uongozi wa timu hiyo ulivyoeleza.
Beki huyo alisema yeye ni mchezaji na ili aweze kufanya kazi yake vizuri, ni vyema uongozi ukatimiza mahitaji yake ambayo walikubaliana.
"Waambie (viongozi) wanilipe mshahara wangu wa miezi minne, ni rahisi nitaondoka, (***’tusi’)," aliandika beki huyo wa timu ya Taifa ya Togo akiwajibu mashabiki wa wanaodaiwa kuwa wa Yanga ambao wanamtaka aondoke kwenye timu yao.
Mtogo huyo, tayari ameshaonyesha mipango yake ya kuachana na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kugoma kusaini mkataba mpya mapema mwaka huu kama alivyotakiwa na uongozi.
Nyota wengine ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu na wamekaa mguu ndani mguu nje ni pamoja na mshambuliaji wa kimataifa kutoka Zimbabwe, Donald Ngoma na winga Simon Msuva.