NYOTA saba wa Simba waliokuwa kwenye timu zao za taifa, wametua kininja mjini Bukoba kuungana na wenzao kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar, Jumapili hii.
Wachezaji hao ni mshambuliaji, Laudit Mavugo, aliyekuwa na kikosi cha timu yake ya Taifa ya Burundi, huku wengine Ibrahimu Ajib, Shiza Kichuya, Jonas Mkude, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Said Ndemla na Muzamiri Yassini, nao wameungana na wenzao baada ya kuiwakilisha Taifa Stars kwenye mechi mbili za kirafiki.
Nyota hao baada ya mechi ya juzi ya kirafiki kati ya Tanzania na Burundi ambapo Stars ilishinda mabao 2-1, jana alfajiri waliondoka jijini Dar es Salaam na kutua mjini Bukoba asubuhi na mapema wakitumia ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na mara baada ya kutua waliungana na wenzao kambini bila hata kupumzika na kwenda moja kwa moja mazoezini kwenye Uwanja wa Taasisi ya Kanisa Katoliki mjini humo.
BINGWA limenasa taarifa za ndani kwamba wachezaji hao waliwekwa mafichoni na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, baada ya kumaliza mechi dhidi ya Burundi kukwepa hujuma kabla ya kuondoka nao.
Kutua kwa wachezaji hao Bukoba kumeleta hamasa kubwa kwa nyota wengine ambao walikwishatangulia na kocha wao Joseph Omog, hivyo waliendelea na maandalizi ya mchezo huo utakaochezwa siku hiyo ya Jumapili kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
“Wachezaji wetu wameingia leo asubuhi kama maninja wakiwa na Kaburu, walipofika tu kitu cha kwanza cha kufanya walibadili nguo na kuungana na wenzao mazoezini,” kilisema chanzo kimoja cha habari cha ndani.
“Ujio wao uliamsha hamasa sana, kwani baada ya kuonekana wenzao waliwafurahia na kuwashangilia na kukumbatiana wakipongezana kwa kile ambacho kila mmoja ameonyesha kwenye mechi hizo za kirafiki,” kiliongeza chanzo hicho.
Meneja wa timu hiyo, Mussa Hassan ‘Mgosi’, ameliambia BINGWA jana kuwa kurejea kwa wachezaji wote saba salama kumeongeza chachu ya ushindani baina yao kuelekea mechi zao za Kanda ya Ziwa wakianza na Kagera Sugar.
“Wachezaji hao wamefika leo asubuhi (jana) na walipata nafasi ya kufanya mazoezi pamoja na wenzao ambao walitangulia kufika hapa, kurejea kwao kumeongeza mzuka na hatuna shaka ya pointi tatu zitapatikana Jumapili,” alisema.
Vinara hao wa Ligi Kuu, Simba itakuwa Kanda ya Ziwa kucheza mechi tatu mfululizo, ambapo Jumapili wataanza na Kagera Sugar mjini Bukoba, kabla ya kwenda Mwanza kukipiga na Mbao FC, kabla ya kuhitimisha ziara hiyo dhidi ya Toto Africans.
Simba inaongoza msimamo wa ligi wakiwa na pointi 55, huku mahasimu wao, Yanga wakishika nafasi ya pili kwa kuzidiwa pointi mbili, wakati Azam ni watatu wakiwa na pointi 44, kila mmoja akiwa amecheza mechi 24.
Credit - Bingwa