Nyakati Hufundisha Elimu Kubwa Sana..Usitumie Nguvu Kubwa Leo Kumkomoa Mwenzako

Ione dunia ilivyo kigeugeu. Leo hii bilionea wa dola, siyo shilingi, Yusuf Manji hana pesa. Manji hana pesa leo?

Inawezekana ni upepo mbaya ambao unavuma kwake kwa muda mfupi kisha utapita na atarejea kwenye kiwango chake. Ila lipo swali; lini uliwahi kuwaza kuwa Manji atakuwa hana pesa.

Leo hii gazeti lake, Jambo Leo halijachapwa kwa siku ya sita sasa. Sababu ni moja tu, hakuna pesa! Manji hana pesa? Hata ya kuchapa gazeti?

Kuna wamiliki wengi wa magazeti, wanayaendesha kwa fedha za kuungaunga lakini hata mara moja hayajakatika sokoni. Leo Manji mwenye fedha isiyo na wasiwasi gazeti lake halichapwi kwa sababu ya kukosa fedha?

Siingii kwenye visanga kuwa akaunti za Manji zimezuiliwa na Serikali ndiyo maana hali ni ngumu, isipokuwa hali hii ambayo anakutana nayo Manji ni elimu kubwa ya nyakati.

Soma nyakati na mabadiliko yake, zingatia IPO KESHO. Unaweza kuwa tajiri mkubwa lakini ukiingia nyakati mbaya utajiri wako usikusaidie.

Soma nyakati na mamlaka. Unaweza kuwa kiongozi mwenye mamlaka makubwa, kisha ukaingia nyakati mbaya, madaraka hayatakusaidia.

Ishi vizuri, tumia utajiri wako vizuri, usitumie mamlaka yako kuonea watu. Dunia haisimani. Soma elimu ya nyakati.

Usilewe madaraka ukadhani nyakati hazitabadilika. Usilewe utajiri ukafikiri kesho haitafika.

Tusome elimu ya nyakati ili kujifunza unyenyekevu, nidhamu na uvumilivu. Leo isikudanganye, kesho itafika ndugu yangu, na ikifika haitakuwa sawa na leo.
Hili somo ni kubwa sana, tuendelee kujifunza, tulielewe na tuliishi. Usitumie nguvu zako za leo kukomoa wenzako, kesho itafika na hizo nguvu hutakuwa nazo, je, utakuwa mgeni wa nani?

Ndimi Luqman MALOTO
Tags

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Maneno kuntu kabisa. Ahsante Maloto

    ReplyDelete
  2. kweli,huyu mama amesomesha mabinti wengi sana hasa yatima.

    ReplyDelete
  3. Mungu yupo ni kuzidi kumuomba tu,kwa sababu hata kama kuna kosa lakini ukatubu kwa dhati,atakuepusha na yote na yataisha,na hakuna lisilo na mwisho,iko siku itabaki kuwa historia isiyofutika.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad