Nyundo 5 za JPM Mtego kwa Vigogo..!!!


RAIS John Magufuli jana aliwaapisha rasmi Dk. Harrison Mwakyembe na Prof. Palamagamba Kabudi kuwa mawaziri kutokana na mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri aliyoyafanya juzi huku akitoa maelekezo matano muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na kila kiongozi nchini.

Magufuli aliwaapisha mawaziri hao Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Dk. Mwakyembe akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushika nafasi ya Nape Nnauye aliyeenguliwa juzi na Prof. Kabudi kushika nafasi aliyokuwa nayo awali Mwakyembe katika Wizara ya Katiba na Sheria.

Wateule wengine walioapishwa na Magufuli jana ni Dk. Abdallah Possi anayekuwa Balozi wa Tanzania nchini
Ujerumani; Sylvester Maselle Mabumba anayekuwa Balozi wa Tanzania nchini Comoro; Alphayo Kidata anayekuwa Katibu Mkuu Ikulu kushika nafasi iliyoachwa na Peter Ilomo aliyestaafu; Job Masima anayekuwa Balozi wa Tanzania nchini Israel na Jaji Stella Mugasha aliyeapishwa kuwa Kamishina wa Tume ya Mahakama.

Baada ya kukamilika kwa kazi ya uapisho iliyokuwa ikisimamiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, ndipo Magufuli aliposhusha ‘nyundo’ hizo tano zinazopaswa kuzingatiwa nao na pia viongozi wengine nchini.

Mambo hayo, ambayo ni wazi kuwa yanaweza kuwa mtego pia juu ya ufanisi wa viongozi wote nchini katika maeneo yao ya kazi, ni pamoja na umuhimu wa kila mmoja wao kujielekeza katika kufanya kazi aliyowatuma.

Pili, kwa mujibu wa nasaha za Rais Magufuli jana, ni kwa kila mmoja wao kutanguliza uzalendo kwa taifa; tatu ni kuwa waumini wa kutenda haki; nne kuwa na ujasiri wa kukabiliana na mizengwe ya aina yoyote katika utekelezaji wa kazi zao na tano; ni kwa kila mmoja kuwa mvumilivu.

Akifafanua, Magufuli alisema mambo hayo ni miongoni mwa sifa muhimu za kila kiongozi.

Magufuli alisema kuwa majukumu yoyote huwa yana lawama, hivyo wasitegemee kusifiwa kwa mazuri hasa kwa nchi kama ya Tanzania ambayo ina baadhi ya watu ambao kazi yao ni kulalamika tu.

“Hayo msiyaangalie. Fanyeni kazi kwa maslahi ya nchi. Mnatakiwa kwenda kusimama imara maana tunapita katika kipindi cha mpito… kutoka katika mazoea ya aina fulani kwenda katika muelekeo fulani,” alisema Magufuli.

UZUSHI KUHUSU KINANA, MWAKYEMBE
Rais Magufuli alisema ameshangazwa na taarifa zilizokuwa zikizagaa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii kwamba Dk. Mwakyembe hatakwenda Ikulu kula kiapo na pia uzushi mwishine kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahmani Kinana, angezungumza na waandishi wa habari ilhali yeye (Magufuli) alimruhusu kwenda India kwa ajili ya matibabu.

“Nashukuru Mwakyembe amekuja kuapa kwa sababu kwenye mitandao walisema hatokuja. Nilikuwa namsubiria nione kama hatakuja na nimemsimamisha kwa makusudi azungumze waone (kuwa) amekuja… wapo watu ambao wangependa Tanzania iangamie. Sijui ni kwa nini?” alihoji.

Alisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuendelea kuchapa kazi na kutokatishwa tamaa na changamoto zozote watakazokutana nazo.

“Hata kwenye vitabu vya dini, hakuna kiongozi ambaye amefanya kazi kwa raha,” alisema, huku akikumbusha kuwa yeye na viongozi wengine wote wapo kwa muda tu madarakani, kama ilivyo kwa uhai wa kila binadamu.

ATOA NENO KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais Magufuli pia alivitaka vyombo vya habari nchini kutumia kalamu vizuri kwa kuitangaza Tanzania kwa sababu matatizo yaliyojitokeza katika nchi nyingine duniani yamechochewa na kalamu zao na kusababisha maafa makubwa.

“Kalamu zikitumika vizuri zitawasaidia Watanzania,” alisema.

Rais Magufuli alisema mara kwa mara kumekuwa na kawaida ya kuandikwa habari za uchochezi ambazo hupewa kipaumbele zaidi na kuonekana ndiyo habari.

“Sasa Mwakyembe kafanye kazi… nataka ukafanye kazi, kama wapo waliokuwapo wanashindwa kuchukua hatua, wewe kachukue. Kwanza ni mwanasheria mzuri, msomi umesomea mambo ya habari.

Kafanye kazi. Serikali ipo. Hatuwezi kuiacha serikali ikiangamia kwa sababu ya watu wachache. Haitawezekana,” alisema.

Rais Magufuli alitoa mfano kuhusiana na jambo hilo kwa kusema: “Kasomeni magazeti, vichwa vya leo… picha za mbele ni za mtu ambaye amefanya kosa moja kana kwamba hicho kitendo kimefanywa na serikali au kinasaidiwa na serikali. Page ya kwanza huyu anatoa anafanya hivi, page ya pili huyu anatoa anafanya hivi… that is the story….nawaambia wamiliki wa vyombo vya habari, be carefull (kuweni waangalifu), kama mnafikiri mna freedom ya aina hiyo."

Akisistiza suala hilo, Rais Magufuli alisema wamiliki wa vyombo vya habari na waandishi wa habari wanatakiwa kuwa wazalendo kwa nchi yao na siyo kutoa kipaumbele kwenye habari za uchochezi ambazo haina maslahi kwa taifa.

Awali, Rais Magufuli baada ya kuwaapisha viongozi hao, alitoa nafasi kwa kila mmoja kuzungumza ambapo Dk. Mwakyembe alisema anashukuru kwa uteuzi huo na kwamba atakwenda kufanya kazi kwa ueledi na kwa kuzingatia nidhamu ya hali ya juu.

Prof. Kabudi alisema uteuzi huo ulimfanya usiku wake kuwa mgumu kwa sababu Rais amempatia heshima kubwa kwa kumuona anafaa na kwamba, atakwenda kufanya kazi kwa kutenda haki.

Dk. Possi alisema atakwenda kuangalia fursa mbalimbali za kiuchumi Ujerumani na kutafuta wawekezaji ili waje kuwekeza nchini.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad