Picha za Nusu Utupu Zawapeleka Polisi Gigy Money, Sanchoka na Amber Lulu

Sekeseke la picha na video za utupu zinazopachikwa na baadhi ya warembo kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram kwa lengo la kujipatia wanaume yaani kujiuza mitandaoni (Cyber Prostitution), linadaiwa kusababisha baadhi yao kuitwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi ‘Sentro’ jijini Dar es Salaam.

TUJIUNGE NA CHANZO CHA NDANI
Kwa mujibu wa chanzo makini cha ndani ya jeshi hilo, warembo hao wanahitajika kwenye Kitengo cha Kupambana na Uhalifu wa Mtandaoni (Cyber Crimes) kilicho chini ya Jeshi la Polisi Tanzania kufuatia video na picha zao za utupu kuendelea ‘kutrendi’ mitandaoni na kumomonyoa maadili ya watoto wa Kitanzania. “Wapo wengi, ni kama ilivyokuwa kwa wale mastaa wa madawa ya kulevya.
Wengi ni hawa warembo, sijui wanawaita video queen. Hawa muda mwingi wapo mitandaoni wanatupia video na picha za utupu. “Polisi wanasema kabla ya sheria kuchukua mkondo wake itabidi wawabane ili kueleza lengo lao ni nini? Kama itabainika wanajua lakini wanafanya makusudi, sheria itachukua mkondo wake na adhabu kali itawahusu.

“Wanaoitwa Sentro wapo wengi lakini kuna huyu Sanchoka (Jane Ramoy), Gigy Money (Gift Stanford) na Amber Lulu (Lulu Auggen). Hawa watoto ni shida hivyo inabidi kuwapunguza spidi na wawe mfano kwa wengine.

YUMO PIA MTANGAZAJI WA REDIO
“Kimsingi hawa ndiyo ambao wamekuwa wakilalamikiwa zaidi. Lakini pia yumo mtangazaji wa redio moja ambaye siku hizi naye anachefua watu na kusababisha watu kuhoji utendani wa kitengo hiki cha polisi.


 Ambacho watu hawakijui ni kwamba polisi hawawezi kumkamata bila kupokea malalamiko kuwa anafanya hiki na hiki mtandaoni na kisheria siyo sahihi. “Lakini kwa hawa malalamiko yapo kila kukicha,” kilinyetisha chanzo chetu.

KWA NINI TCRA HAWACHUKUI HATUA?
Akizungumza na Wikienda juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) juu ya watu kama hao, Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy anafafanua kuwa, mamlaka hiyo haina mamlaka ya kumkamata mtu isipokuwa malalamiko yanapaswa kupelekwa polisi.

“Jeshi la Polisi likishapata malalamiko, wenyewe ndiyo wanajua namna ya kukamata wahusika,” alisema Mungy. Baada ya kuwasikia TCRA, Wikienda lilifika Sentro kwenye kitengo hicho cha uhalifu wa mitandaoni na kuonana na Kamanda wa Kitengo cha Uhalifu wa Mitandaoni (Cyber crimes Unity), Kamanda Mwangasa Joshua ambaye alizungumzia juu ya ishu hiyo.


Kamanda Mwangasa aliliambia Wikienda kuwa, baada ya kupokea malalamiko hayo, jopo lake la wachunguzi limekuwa likizipitia ‘accounts’ zote za warembo hao ili kuwachukulia hatua stahiki haraka iwezekanavyo.

“Sisi kama mamlaka yenye dhamana hatuwezi kuvumilia ukiukwaji wa sheria wa kiwango hicho. Tukishawahoji, tukijiridhisha, tutawafikisha mahakamani mara moja.

“Lakini niwatahadharishe tu kwamba uchunguzi ni muhimu kwa sababu mtu anaweza akatengeneza account kwa jina la mtu mwingine, lakini la kujiuliza hapo mtu huyo anapataje picha zako za utupu kila siku na kuzituma?

“Yote hayo tutayajua tukichunguza. Siwezi kupuuza taarifa tunazozipokea za warembo hao.

“Wananchi wanapaswa waelewe kuwa sheria haikukatazi wewe kupiga picha ya utupu, lakini inakuzuia kutumia picha hiyo vibaya kwa kuituma kwenye mitandao kisha kila mtu akaiona. Hilo ni kosa kisheria, kwa hiyo sisi tutaanza na hao ambao tayari majina yao tunayo.

“Niwashukuru wanahabari kwa kuendelea kutuonyesha uozo unaofanywa na watu mbalimbali ambao wakati mwingine sisi tunakuwa hatuna taarifa zao, sheria ya mtandao haijambagua mtu, sheria hii ipo kwa ajili ya watu wote, haijalishi kama wewe ni mtu maarufu au siyo maarufu, ukifanya kosa utawajibishwa tu,” alisema Kamanda Mwangasa.

GIGY, AMBER WAJITETEA Wikienda liliwatafuta mamodo hao kwa nyakati tofuati ambapo Sanchoka hakuweza kupatikana huku Gigy na Amber Lulu wakijitetea kuwa watajieleza kwamba huwa wanafanya kwa ajili ya matangazo ya nguo.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad