Polisi Waua Wamasai kwa Kuwatwanga Risasi Mchana Kweupe...!!!!


JPM twafa! Ndivyo walivyosikika wafugaji wa jamii ya Kimasai mkoani hapa ambao wamemlilia Rais John Pombe Magufuli kuwa wanauawa kwa uonevu na askari wa Jeshi la Polisi, kufuatia mauaji ya vijana wawili yaliyofanyika Jumanne iliyopita katika oparesheni ya kuwaondoa wafugaji kwenye Kijiji cha Kidomole Kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo.

HIVI NDIVYO ILIVYOANZA

Mchana wa Jumanne hiyo, vijana wawili ndugu wa kuzaliwa, Rumai Kambererega (22) na Sainga Kambererega (25) walikuwa kijijini hapo, walipozaliwa na kukulia, wakichunga mifugo yao na ghafla wakatokea askari ambao walianza kuikamata mifugo yao pasipo maelezo.

Vijana hao walianza kuhoji sababu za askari hao kuikamata mifugo yao, lakini kukatokea hali ya kutokuelewana, ndipo walipoanza kushambuliana, watoto hao wa wafugaji wakitumia silaha zao za jadi aina ya mishale huku polisi wakijibu mapigo kwa kuwafyatulia risasi.

MAPAMBANO YAPAMBA MOTO

Katika tukio ambalo awali lilionekana kama dogo na lingemalizika kirahisi, hali ilibadilika na kufanya mapambano kupamba moto, kitu kilichowalazimisha polisi ambao idadi yao haikufahamika mara moja, kumpiga risasi mbili Sainga, moja ya paja na nyingine chini ya goti, hali iliyopelekea kifo chake baada ya kuvuja damu nyingi.

Kuona kaka yake akianguka na kupoteza uhai mbele yake, Rumai alicharuka, lakini naye alitulizwa kwa kupigwa risasi ya kifua na kusababisha kifo chake hapohapo.

WAMASAI 200 WAKUSANYIKA

Baada ya tukio hilo ambalo liliwaacha askari hao wakikimbia, ghafla wafugaji zaidi ya 200 walijikuta wakikusanyika eneo hilo na silaha za jadi, wakiwasubiri polisi ambao waliamini watarejea tena kwa ajili ya kuchukua miili hiyo kwa ajili ya taratibu za kipolisi.

POLISI WATOKEA, WAPIGWA BITI, WAREJEA WALIKOTOKA

Kama vile walielewa kitakachofuata,  polisi walitokeza eneo hilo la tukio kwa ajili ya kuichukua miili hiyo, lakini wamasai hao wakiwa na jazba, waliwakataza kuigusa, vinginevyo mauaji zaidi yangetokea, isipokuwa wakatakiwa kurejea walikotoka, kuwachukua viongozi wa serikali ili waweze kulimaliza suala hilo.

WAONYESHA MSIMAMO

Wananchi hao walishangazwa na kitendo cha vijana wao kuuawa katika kijiji chao walichoishi kwa zaidi ya miaka 40.

“Tupo katika kijiji hiki kwa zaidi ya miaka 40 tunaishi hapa, tuna hati za utambulisho kama wakazi wa eneo hili, tunaomba rais aingilie kati, tunakufa,” alisema mmoja wa wananchi hao kwa jazba.

MKUU WA WILAYA AWAKANA POLISI

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga alisema ni kweli walikuwa kwenye operesheni za kuwaondoa wafugaji katika baadhi ya maeneo lakini si katika Kijiji cha Kidomole.

POLISI WAREJEA KESHO YAKE

Baada ya polisi hao kugomewa kuchukua miili hiyo, waliondoka ambapo kesho yake (Jumatano) walifika wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Banaventura Mushongi, wakiwa na msafara wa magari matatu ya askari wa kutuliza ghasia pamoja na mengine yaliyowabeba maofisa wa polisi.

Akiwa eneo la tukio, Kamanda Mushongi alizungumza na wafugaji hao waliokuwa wakiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji Tanzania, Alex Masha.

BABA WA MAREHEMU ALIA UONEVU

Katika kikao hicho, baba wa marehemu hao aliyejitambulisha kwa jina la Kambererega Kisamoda alilia uonevu uliofanywa kwa wanaye, akisema wamekufa kikatili wakichunga mifugo katika kijiji walichozaliwa.

“Sasa wanangu hivi wangeepuka vipi hiki kifo jamani, hapa ni kijijini kwao wanafuatwa na kuuawa kinyama hivi, mbona wafugaji tunaonekana kama siyo raia wa nchi hii jamani.

“Kwa kweli tumechoka kuonewa kila kukicha, vifo hivi vya wanangu vinaniuma sana, tena wameuawa wote wawili kwa pamoja, hata mama yao Toroda aliposikia alilia sana na bado analia mpaka sasa, tunaomba rais wetu Magufuli atusaidie haki ipatikane,” alisema.

RPC AVUA MAGWANDA, AVAA UDIPLOMASIA

Katikati ya watu wenye simanzi na jazba, Kamanda Mushogi, alijishusha kutoka uaskari na kuwa msuluhishi, akitumia busara ya hali ya juu kuwatuliza raia hao kila walipotaka kupandisha mori, akisema kila tatizo huwa na mwisho hivyo watulie kwani hata tatizo lililo mbele yao, litatatuliwa na uvumbuzi kupatikana.

Mamia ya raia waliojaa kwenye kikao hicho wakiwa na jazba, walianza kuinua mikono wakitaka kumuuliza maswali RPC huyo, huku wakikumbushia kifo cha mfugaji mwenzao mwingine, aliyepigwa risasi Agosti, mwaka jana ambapo waliambiwa na Mkuu wa Mkoa Evarist Ndikilo kuwa waliofanya mauaji hayo wangechukuliwa hatua, lakini hakuna chochote kilichofanyika.

Akijibu swali hilo, RPC Mushongi aliwaambia wafugaji hao kuwa kesho yake (Alhamisi) angerudi tena mahali hapo kufanya nao kikao akiwa pamoja na Ndikilo.

WAFUGAJI WATULIA, WARUHUSU MIILI KUCHUKULIWA

Baada ya kuelewa somo la busara kutoka kwa RPC Mushongi, walimruhusu aichukue miili ya marehemu hao na kwenda kuhifadhi hospitali wakati uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea

Miili ya marehemu hao ilichukuliwa majira ya saa kumi na mbili za jioni na kwenda kuhifadhiwa Hospitali ya Bagamoyo na kufanyiwa uchunguzi.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. waliohusika waondoke ofcn na kuchukuliwa hatua kali...fidia na uhakiki wa usalama wao uwekwe wazi..duu..mtu amepoteza watoto wawili?acheni majibu rahisirahisi..vaeni viatu vya huyu baba..

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad