Akiendelea na ziara yake mkoani Lindi, Rais Dkt Magufuli amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo na kutoa maagizo ili kuhakikisha wananchi wananufaika na jitihada za serikali za kuboresha maisha yao.
Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kumnyang’anya pasi ya kusafiria (passport) Mkandarasi anayeshughulikia Mradi wa Maji wa Ngapa hadi hapo atakapokamilisha mradi huo.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo alipokwenda kukagua mradi huo wa maji ambao hadi sasa umetumia miaka 6 kujengwa lakini bado haijakamilika. Pamoja na kuagiza pasi ya mkandarasi ichukuliwe, Rais Magufuli amempa miezi miwili mkandarasi huyo kuhakikisha mradi unakamili huku RC Zambi akiwa na jukumu la kuhakikisha kuwa mkandarasi hatoki eneo hilo la mradi.
Mradi huo unaotarajiwa kumaliza tatizo la maji mkoani Lindi umegharimu TZS bilioni 29 ambapo hadi sasa mkandarasi amelipwa bilioni 21. Rais Magufuli amesema kuwa kama tatizo ni fedha ndio sababu mradi haumaliziki aambiwe ili atoe fedha serikali kuu kukamilisha wananchi waweze kupata maji.
Mradi huo wa maji ukikamilika unatarajiwa kuzaliwa maji zaidi ya lita milioni 6 kwa siku.
Rais Magufuli anatarajiwa kukamilisha ziara yake mkoani Lindi leo jioni ambapo ataanza safari ya kwenda mkoani Mtwara atapofanya ziara yake Jumamosi na Jumapili. Katika kuhitimisha ziara yake ya siku nne katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara, Rais Magufuli atahutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.