AMA kweli Emmanuel Okwi amenogewa na Simba, kwani licha ya uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi kuweka wazi kuwa atarejea msimu ujao, taarifa kutoka Uganda zinadai kuwa, hata yeye mwenyewe ameonyesha mapenzi ya kurejea kwenye timu yake hiyo ya zamani.
Okwi, ambaye alikuwa akikipiga nchini Denmark katika Klabu ya SonderjyskE, kwa sasa anaichezea SC Villa ya nchini kwao Uganda na anafanya mambo makubwa, hali iliyomfanya kuitwa kwa mara nyingine katika kikosi cha timu ya Taifa ya nchi hiyo.
Miongoni mwa marafiki wa Okwi kutoka nchini Uganda, amesema kuwa, mchezaji huyo anasubiri tu kumalizika msimu huu arejee Tanzania kujiunga na Simba, baada ya viongozi wa timu hiyo kuonyesha nia ya kumhitaji.
“Hata yeye mwenyewe anaipenda Simba, kwa sasa baada ya kusikia kuwa viongozi pamoja na mashabiki wanataka arejee, anajiandaa kumalizia msimu huu na kuna kila dalili wakamalizana mapema,” alisema rafiki huyo wa karibu.
Kwa upande wake, Kocha wa zamani wa Simba, ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Uganda, Mosses Basena, alisema kuwa, Okwi amekuwa akionyesha kiwango kizuri kila siku, hivyo kama Simba atamrejesha watakuwa wamelamba dume.
Mapema Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, aliliambia gazeti hili kuwa, suala la Okwi wala halina mjadala mkubwa, kwani yeye kwa klabu hiyo ni kama nyumbani, hivyo anakaribishwa muda wowote.