MAKAMU wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, ameonekana kuwaweka gizani mashabiki wa Yanga kutokana na kitendo chake cha kila wakati kumtaja Mganda Emmanuel Okwi.
Okwi ni miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwatia tumbo joto Yanga, zaidi ikiwa ni kutokana na kile alichowafanyia wakali hao wa Jangwani Septemba 2012 alipoiongoza Simba kuwapiga watani wao hao wa jadi mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa kufahamu hilo, kwa muda wote ambao Okwi amekuwa nje ya kikosi cha Simba, mabosi wa klabu hiyo wamekuwa wakilitaja jina lake kwamba wapo mbioni kumrejesha kama sehemu ya kuwatisha Yanga.
Hali hiyo ilijirudia kwa mara nyingine juzi kupitia kwenye mitandao ya kijamii, ambapo Kaburu aliposti video ya mechi waliyoichapa Yanga mabao 5-0 na kuweka ujumbe uliosomeka: ‘Usiyemtaka anakuja’.
Ujumbe huo ulionekana kama kutuma salamu Yanga kwa wakati huu ambao timu hizo zinafukuzana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba ikiwa kileleni kwa pointi zake 55, huku wapinzani wao hao wakifuatia na pointi 53.
Kwa muda mrefu kumekuwa na tetesi kuwa Okwi anatarajiwa kurejea Msimbazi baada ya klabu yake hiyo ya zamani kumalizana na SC Villa ya Uganda anayochezea kwa sasa.
BINGWA lilizungumza na Kaburu kuhusu mchezaji huyo ambapo alisema, Kamati ya Utendaji ya Simba haina pingamizi kuhusu usajili wa Okwi kama benchi la ufundi litahitaji huduma yake.
Alisema kwa muda ambao Okwi ameishi na kutumikia kikosi cha Simba, hawana wasiwasi naye na kwamba Msimbazi ni sawa na nyumbani kwa Mganda huyo.
“Okwi, Simba ni nyumbani kwake, kama kocha atahitaji huduma yake, basi hatuna pingamizi,” alisema Kaburu.
Credit - Bingwa