Uongozi wa Clouds Media Group umesema utachukua hatua ukituhumu wafanyakazi wake kuvamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye aliambatana na polisi wapatao nane, wengi wao wakiwa na silaha za moto. Taarifa zilieleza kuwa, Makonda alivamia ofisi za Clouds, usiku wa kuamkia juzi na kutoa vitisho kwa watangazaji na waongozaji wa Kipindi De Weekend Chat Show maarufu kama Shilawadu.
RUGE AFUNGUKA
Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba, jana aliliambia Wikienda katika mahojiano maalum kwamba, hakuna aliyepigwa kati ya wafanyakazi hao, lakini uvamizi huo uliambatana na vitisho vikali.
“Ni kitu ambacho kinatusikitisha sana, vimefanyika vitisho ikiwa ni pamoja na mheshimiwa (Makonda) kuondoka na baadhi ya clip (kipande cha video),” alidai Ruge.
Ruge alisema kuwa, wanalaani vikali kitendo hicho alichokiita cha unyanyasaji, chenye lengo la vitisho kwao na uhuru wa habari.
Wikienda: Kisa hasa cha kuvamiwa ni nini?
Ruge: Unajua Shilawadu walifanya mahojiano na yule mama anayedaiwa kuzaa na Gwajima (Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima). Lakini mimi niliona ile stori inakosa mambo mengi ya weledi. Nikaizuia isiende hewani na wale vijana hawana makosa kwa kuwa mimi ni kiongozi wao ninayetaka uhakika wa mambo.
Wikienda: Kwa nini alivamia huo usiku?
Ruge: Alihoji kwa nini ile ishu ya Gwajima haijarushwa. Wakamuambia ni bosi Kusaga (Mkurugenzi wa Clouds Media Group) amewakataza, nafikiri walichanganyikiwa kwa sababu ya vitisho, unajua ni vijana wadogo na wale wamebeba bunduki zaidi ya moja. Ila mimi ndiyo nilikataza kama nilivyokuambia.
Wikienda: Kuna madai aliondoka na baadhi ya vitu vya ofisi, ni kweli? Ruge: Aliondoka na clip (kipande cha video) ya mahojiano ya yule mwanamke. Nafikiri baada ya hapo imeanza kusambaa mitandaoni.
Wikienda: Umesema vijana wamepata mshtuko wa kisaikolojia, tunaweza kuongea nao?
Ruge: Kwa kweli hatuwezi kukuruhusu. Tuwaache wapumzike, hawako vizuri na unajua walichanganyikiwa.
Wikienda: Kuna taarifa wewe uliwasiliana na Gwajima ndiyo ukaizuia isionyeshwe?
Ruge: Gwajima niliwasiliana naye mara tatu, lakini alikuwa akinieleza namna kulivyo na njama za makusudi kumchafua. Baada ya hapo tulifanya uchunguzi na kuona kweli kuna shida.
Wikienda: Leo (jana), ulishikiliwa na polisi?
Ruge: Sikushikiliwa lakini nilikwenda Oysterbay Police Station kwa ajili ya kutoa maelezo kuhusiana na jambo hili. Wikienda: Kuna taarifa wanasheria mmewaweka tayari kufungua kesi, je, ni kweli? Ruge: Tumefanya mazungumzo na wanasheria wetu kama kujua nini cha kufanya. Tumekuwa na vikao kutwa nzima. Lakini wako wanasheria wengi wamejitolea, tena bure kulisimamia suala hili kisheria.
Wikienda: Kuna taarifa nyingine zimesambaa kwamba Makonda alikuja kuwatembelea tu kwa kuwa ana documentary yake ya mwaka mmoja wa uongozi wake alikuja kuikagua tu, je, ni kweli?
Ruge: Uzushi mtupu, kuna watu wamekuwa wakifanya juhudi za kutaka kulibadilisha hili. Wanataka lionekane ni jambo la kawaida na ilikuwa hivyo. Lakini ukweli ni ule niliokueleza. Watu hawajui, Clouds ni taasisi ya watu wenye ushirikiano wa juu kabisa. Hatuwezi kukubali kuchezewa hivi na tukakaa kimya au kukubali kubadili mambo kirahisi namna hii. Jiulize, kuna clip moja ya pale mapokezi ambayo wameiona, jengo la Clouds Media lina CCTV kila sehemu. Unafikiri clip nyingine zinaonesha nini? Wanataka kupindisha, wanajua kuna nini?
Wikienda: Taarifa za Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuja Clouds kuhusiana na tukio hili, je, ni kweli?