Sakata la Kupotea kwa Msaidizi wa Mbowe Lafikia Hatua Hii,Mapya Yaibuliwa...!!!


MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boaz, amesema mpaka sasa ofisi yake haijafanikiwa kupata taarifa za kuisaidia kujua kilichompata Ben Saanane, Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Aidha, Kamishna Boaz amesema ofisi yake imetoa taarifa kwa kutumia mfumo wa kiuchunguzi kwa Jeshi la Polisi la Kimataifa (Interpol) kumsaka mwanachama huyo wa Chadema, lakini bado halijapata mrejesho wowote.

Saanane anadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha na hajawahi kuonekana tangu Novemba mwaka jana, takribani miezi mitano sasa.

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki kuhusu suala hilo, Kamishna Boaz alisema licha ya taarifa nyingi walizozipata kutoka kwa watu mbalimbali juu ya kupotea kwa mwanachama huyo wa Chadema, hakuna hata moja iliyotoa mwanga wa kupatikana kwake.

Alisema mpaka sasa wameshawahoji watu wote ambao kwa namna moja ama nyingine walionekana kuwa karibu na Saanane.

Kamishna Boaz alisema wamewahoji pia watu wote waliokuwa wanazungumzia suala hilo katika vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali, lakini hakuna mafanikio yoyote waliyoyapata kwenye msako wa mwanachama huyo wa Chadema.

"Uchunguzi wa Saanane bado unaendelea, na tunachunguza taarifa zote tunazopatiwa, lakini mpaka dakika hii hatujaweza kupata taarifa nzuri ambazo zinaweza kutusaidia yuko wapi au kuna nini kimemkuta mpaka asionekane," Kamishna Boaz alisema.
"Tunaendelea kukaribisha taarifa kwa mtu yeyote ambaye anaweza kusaidia katika uchunguzi huu."

UCHUNGUZI KIMATAIFA
Kamishna Boaz alisema mbali na kuhoji vyanzo mbalimbali vya ndani ya mipaka, ofisi yake pia imeshatoa taarifa kwa kutumia mfumo wa kiuchunguzi kwa Jeshi la Polisi la Kimataifa (Interpol), lakini bado hawajapata mrejesho wowote.

"Kama mtu amepotea na taratibu zote tumeshazifanya hakuna mafanikio, tunaendelea kuwaomba watu watupe taarifa," alisema.

"Kwa mfano, tunapomtafuta mtu huwa kuna fomu maalumu tunajaza ambayo inaonyesha huyo mtu alikuwa anafananaje, anavaaje, tunaweka picha yake, anapenda kutembelea wapi, na huwa tunazisambaza katika maeneo tofauti, yote hayo tumefanya.

"Na hata Interpol huwa tunatangaza na ambacho huwa kinafanyika ni kuweka taarifa za mtu kwamba tunamtafuta ni ‘missing person’ (mtu aliyepotea).

"Kwa hiyo, inaweza kutokea kwa mfano kama ni mtu amekwenda nchi za nje kwa njia moja ama nyingine kutokana na utaalamu uliopo anaweza akapatikana.

"Taratibu zote hizo tumeshafanya, lakini mpaka sasa hatujapata mrejesho wowote."

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho cha siasa, Tundu Lissu, Saanane aliwasiliana kwa mara ya mwisho na Mbowe Novemba 14, mwaka jana na tangu siku hiyo, hawajawahi kupata mawasiliano yake ya simu na hajulikani aliko.

Matukio ya wanasiasa kupotea nchini ni nadra, ingawa Juni 12 mwaka jana, chama cha ACT-Wazalendo kilidai kiongozi wake mkuu, Zitto Kabwe alikuwa hajulikani alipo kwa zaidi ya saa 12.

Msafiri Mtemelwa, Kaimu Katibu Mkuu wa ACT, alidai Zitto alikuwa akitafutwa na Polisi tangu usiku wa kuamkia siku hiyo na kwamba "mpaka sasa hatujui kiongozi wetu yupo wapi na yupo kwenye hali gani. "Askari kanzu wanalinda nyumbani kwake na kwa watu wake wa karibu. Sisi kama chama tunaliambia Jeshi la Polisi kuwa lolote litakalotokea kwa kiongozi wetu wao watajibu kwa umma."

Zitto aliibuka siku mbili baadaye, hata hivyo, na kusema yuko salama wa afya huku akilaani mbinu za Jeshi la Polisi kutaka kumkamata kwa siri bila kufuata utaratibu unaotakiwa.

"Ilikuwa Jumamosi, walikuja nyumbani kwangu wakiwa na magari matatu ila hawakufanikiwa, siwezi kukamatwa kwa 'terms' (matakwa) zao," alisema Zitto, "ila nitakuwa tayari kukamatwa kwa 'terms' zetu na wala siyo kuviziana.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad