Serikali Ivunje Ukimya Kuhusu Manji


Hakuna taarifa rasmi kutoka vyombo vya usalama kuhusu Manji, zaidi ya ile ya uhamiaji kuwa walikuwa wakimsubiri atoke hospitali Muhimbili ili wamlaze mahabusu. Wakati huo Manji alikuwa amelazwa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Manji alilazwa Muhimbili baada ya kuzidiwa akiwa mahabusu Kituo Kikuu cha Polisi (Central), Dar es Salaam, alipowekwa mahabusu baada ya kutajwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya, ingawa alifunguliwa kesi ya kutumia na siyo kuuza.

Habari zinasema Manji anaumwa matatizo ya moyo na amelazwa hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Wakati huohuo, zipo habari kuwa akaunti zake zimezuiwa. Nyingine zinasema Manji amekutwa na uraia wa nchi mbili.
Kampuni zake zinashindwa kujiendesha. Gazeti lake la Jambo Leo halijachapwa na kuingia mitaani kwa wiki nzima sasa. Angalau hili linathibitishika kwa urahisi.

Hapa ndipo kwenye utata kuhusu Manji na lazima tujadili kwa sababu Manji akiathirika, wanaothirika ni Watanzania wengi mno ambao maisha yao yapo kwenye ajira kupitia kampuni za Manji.

Shida ni kuwa Serikali haisemi kitu. Je, watu wa Manji wanaisingizia Serikali, kwamba yenyewe haijafunga akaunti hata moja ya Manji? Serikali inatakiwa itoke na kukanusha kusingiziwa huku.

Kama ni kweli akaunti za Manji zimezuiwa, maana yake hiyo ni kesi nzito mno. Na inapaswa kuelezwa kinagaubaga ili Watanzania wengine wajue kuwa nini ambacho kinamsibu Mtanzania mwenzao. Izingatiwe kuwa Manji ni mwekezaji mkubwa nchini.

Maana kama ni ile kesi ya uhamiaji mbona watuhumiwa walishapandishwa kizimbani na dhamana yao kuwekwa wazi?

Kilichosababisha akaunti za Manji zizuiwe ni nini? Je, ni ile kesi yake ya matumizi ya dawa za kulevya au ya uhamiaji? Mbona kesi hizo hazina uzito wowote wa kusababisha akaunti za mfanyabiashara mkubwa kama Manji zifungwe?

Nini kimesababisha? Serikali iseme, kufanya vitu kimyakimya si vizuri kwa uendeshaji wa nchi. Manji ni Mtanzania, hata kama angekuwa siyo Mtanzania, vema kama anakuwa na matatizo ya kisheria yasemwe na mchakato uonekane ukitendeka.

Serikali ijiepushe na nyenendo ambazo itaonekana inafanya vita binafsi na raia wake.

Ndimi Luqman
@luqmanmaloto
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Kama kweli akaunti za Manji zimefungiwa basi serikari inapaswa kuueleza umma wa watanzania nin sababu ya kufungia akaunt hizo kwa maana makosa aliyokamatiwa hayahusian na ukwepaji wa kodi kosa ambalo linaweza pelekea kufunga akaunt ya mtu. Kama ni ishu za kisiasa basi kunapaswa kutafuta njia njingine ya kumnyon'gonyesha na si kuathiri maisha ya watanzania wengine wengi wanaomtegemea manji kulisha familia zao na tegemezi wao.

    ReplyDelete
  2. Tatizo watanzania kila mtu anajifanya anajua kuongea, hata mambo ya msingi mnataka msingizie siasa, hakuna mtu aliye juu ya sheria, huyo Manji asishitakiwe yeye nani? acheni kujidunisha na mazoweya, ukikiuka sheria sheria itachukua mkondo wake.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad