SERIKALI imesema itatoa zawadi ya Sh. 500,000 kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa na kushtakiwa kwa mtu yeyote mwenye kiwanda au mtambo wa kuzalisha pombe za viroba ambayo haitambuliki na serikali, atapata zawadi ya Sh. milioni moja.
Pia kwa mtu atakayetoa taarifa ya kusaidia kukamatwa kwa mtu yeyote mwenye ghala au aliyehifadhi shehena ya pombe za viroba atazawadiwa Sh. 500,000.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira pia ilieleza kuwa kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa ya kuwezesha kukamatwa kwa mtu au watu wanaoingiza nchini pombe hiyo kutoka nje ya nchi, atazawadiwa Sh. 500,000.
“Kwa atakayetoa taarifa itakayowezesha kukamatwa na kushtakiwa mtu anayezalisha, anayeuza au kutumia stempu feki za TRA, atapata zawadi ya shilingi milioni moja", iliongeza taarifa hiyo na kudadavua kuwa taarifa zitolewe kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno au WhatsApp au kwa kupiga simu namba 0685 333 444.
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa tangu kuanza kwa operesheni Machi 3 hadi 4, mwaka huu, viwanda 16 vinavyojihusisha na uzalishaji wa pombe hizo, maduka 18, maghala manne, baa tatu vilikaguliwa.
Kadhalika, ilieleza kuwa katika operesheni hiyo, katoni 99,171 za pombe kali za viroba zilikamatwa.
Ilieleza kuwa bidhaa za pombe kali zilizofungashwa katika vifungashio vya plastiki zenye ujazo mdogo wa thamani ya Sh. bilioni 10.8, zilikamatwa na kuzuiliwa katika maduka.
Taarifa pia ilieleza kuwa operesheni ya kukamata pombe za viroba itaendelea nchi nzima huku ikizitaka kamati za ulinzi na usalama za mkoa, wilaya hadi ngazi ya vijiji kuhakikisha zinashirikiana na wenyeviti wa mitaa na vijiji katika kutokomeza bidhaa hizo.
“Kamati za ulinzi na usalama za mikoa, zinawajibika kuwasilisha taarifa za operesheni wakati na baada ya operesheni Ofisi ya Makamu wa Rais kila mara kwa kufuata maelekezo yatakayotolewa,” ilisisitiza taarifa hiyo.
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais iliwataka viongozi hao kufungua kesi mahakamani dhidi ya wafanyabiashara waliokiuka katazo hilo ili adhabu kali zitolewe dhidi yao.
Vile vile, viroba vyote vilivyokamatwa pamoja na mizigo mingine, iendelee kubaki chini ya ulinzi kwa sheria zilizotumika na mtu yeyote asiruhusiwe kufanya chochote hadi maelekezo zaidi yatakapotolewa na serikali.