Maombi ya mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuph Manji dhidi Idara ya Uhamiaji yamechukua sura mpya baada ya Serikali kutakiwa iwasilishe kiapo kinzani za majibu.
Mahakama imeagiza Serikali ifanye hivyo ifakapo Jumatatu ijayo na imepanga kusikiliza maombi hayo siku hiyo.
Manji amefungua maombi hayo katika Mahakama Kuu akihoji uhalali wa kushikiliwa na idara hiyo huku akiwa bado amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam kwa matibabu.
Uhamiaji inamtuhumu mfanyabiashara huyo kuwa siyo raia wa Tanzania.
Agizo dhidi ya Serikali la kuwasilisha hati ya kiapo kinzani ikiwa ni majibu limetolewa na Jaji Ama-Isario Munisi anayesikiliza maombi hayo.
Katika maombi hayo aliyoyafungua kupitia Wakili wake, Hudson Ndusyepo, Manji anaiomba Mahakama Kuu iiagize Uhamiaji imfikishe mahakamani ili iamue uhalali wa kushikiliwa kwake na kisha iamuru aachiwe huru.