NAPE Nnauye, jana ameondolewa kwenye nafasi yake ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kufuatia mabadiliko madogo yaliyofanywa katika Baraza la Mawaziri na Rais John Pombe Magufuli.
Ingawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayo mamlaka ya kufanya uteuzi wa nafasi yoyote wakati wowote kwa mujibu wa katiba, tukio la kuondolewa kwa Nape, limepokewa kwa mshtuko mkubwa na tasnia ya Habari nchini, hasa kwa kuwa alionekana dhahiri kuwa pamoja nao katika kipindi hiki ambacho wametikiswa.
Nape, mtoto wa kada wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Brigadia Moses Nnauye, aliteuliwa katika Baraza la Mawaziri la Kwanza la Rais John Magufuli Desemba 9, 2015 kushika wadhifa huo. Hadi jana wakati akiondolewa ofisini, Nape anakuwa amehudumu katika uongozi huo kwa siku 467, huku akionekana kama mtu ambaye alitekeleza majukumu yake kwa namna ya kipekee, kwani kwa muda wote huo, aliweza kukutana, kujadili na kutoa maamuzi mazuri kwa watu wote waliohusika na wizara yake.
Ingawa wizara yake ilihusika na wanamichezo, wasanii, wana utamaduni na wanahabari, lakini ni watu wa kundi la mwisho ndilo waliopatwa na mshtuko mkubwa, hasa kwa kuangalia siku zake tano za mwisho akiwa kiongozi, jinsi alivyoshirikiana nao katika tukio kubwa na baya kuwahi kuitokea tasnia ya habari Tanzania.
Ijumaa ya Machi 17, 2017 usiku, chumba cha habari cha televisheni ya Clouds kilivamiwa na askari, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye alikwenda studio na kuwatisha watangazaji, kwa kitendo chao cha kushindwa kurusha habari iliyokosa vigezo, iliyomhusu Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Tukio hilo lilibakia kuwa siri ya kituo hicho hadi video fupi ilipovuja, Jumapili Machi 19, 2017 na kuzua mjadala mkubwa mitaani na kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, kitu kilichomuibua Waziri Nape ambaye kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter, alisema kama Waziri anayehusika na habari, angekwenda kesho yake, Jumatatu katika ofisi hizo ili kujua kilichotokea. Jumatatu ya Machi 20, 2017 Waziri Nape alikwenda Clouds kama alivyoahidi na huko akakutana na uongozi wa Clouds Media Group, chini ya Mkurugenzi wake Mtendaji, Joseph Kusaga na kufanya mazungumzo.
Pia alikuwepo Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi ambaye ni Mwenyekiti wa chombo cha wamiliki wa vyombo vya habari, MOAT. Akionekana mtu aliyesikitishwa na tukio hilo, Nape aliteua Kamati ya watu watano, ikiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Dk.
Hassan Abbas ili kutafuta ukweli wa tukio hilo na kuwapa saa 24 ili wakamilishe ripoti yao. Jumanne, Machi 21 waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari walikusanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) barabara ya Sam Nujoma kusikia kilichosemwa na Kamati, lakini hakukuwa na chochote, kiasi kuzua minong’ono kuwa ‘wakubwa’ wamezuia ripoti hiyo, jambo ambalo lilikanushwa na Nape, aliyetaka kuwepo kwa subira, kwani kamati yake ilikuwa bado kazini.
Jumatano, Machi 22, 2017 katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) Waziri Nape alipokea ripoti ya kamati hiyo, ambayo kabla ya kukabidhiwa, ilisomwa hadharani na Katibu wake, Deodatus Balile. Akiipokea ripoti hiyo, Nape alisema imemsikitisha na akawataka viongozi kuwa na ngozi ngumu, hasa wanapoongoza watu.
Alisema yeye sio mtu wa kutoa uamuzi juu ya suala hilo, isipokuwa ripoti hiyo ataiwasilisha kwa mamlaka ya juu yake, ambao ni Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao ndiyo wenye mamlaka ya maamuzi.
Jumatano, Machi 23, 2017 taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ilisema Rais John Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri, kwa kumteua Dk. Harrison Mwakyembe kuwa mbadala wa Nape, huku nafasi yake yeye (Mwakyembe) ikichukuliwa na Profesa Paramagamba Kabudi. Maisha kweli hayatabiriki, anyway, Karibu Mheshimiwa Harrison Mwakyembe, uanzia pale alipoacha Nape Nnauye!