DAR ES SALAAM: Inauma sana jamani! Mtoto Queen Carlos miaka 6 tu aliyekuwa akiishi na mama yake mzazi maaneo ya Vatican Sinza jijini hapa, Machi 13, mwaka huu, maiti yake ilikutwa ndani ya gari bovu lililokuwa gereji kwa matengenezo.
Tukio hilo liliacha simanzi kwa familia, ndugu na majirani baada ya mtoto Queen aliyekuwa akisoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi, Sinza Mihogoni, kubainika amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.
MAITI ILIVYOKUTWA
Mwili wa marehemu Queen ulikutwa umekuwa umekaa kwenye siti ya nyuma ya gari hilo aina ya Hyundai na kama mtu angemwona kwa mbali, angejua mtoto huyo alikuwa amelala tu na muda wowote angeamka na kurudi nyumbani kwa mama yake!
MADAI ILIVYOKUWA
Mtu mmoja aliliambia Amani kuwa, siku hiyo mmiliki wa gari hilo alikwenda kulichukua gari lake ili kulipeleka sehemu nyingine, hivyo alifuatana na dereva ambaye angekuwa kwenye gari hilo bovu huku mmiliki huyo akiliendesha gari la kuvuta.
“Walipofika, walifunga kamba ya kuvutia, dereva akaingia kwenye gari la kuvutwa lakini alibaini kuwa, anasikia harufu mbaya. Mmiliki akamwambia lazima kuwa na harufu mbaya kwa sababu gari lilikaa muda mrefu pale gereji. Gari lilipotoka nje ya gereji ikaonekana haliwezi kutembea kwenye lami kwa sababu matairi yote hayakuwa na upepo.
“Sasa katika kuangalia nini wafanye kuhusu upepo ndipo yule dereva akaona mwili wa marehemu umekaa siti ya nyuma, akapiga kelele na watu wakafika,” alisema mtu huyo akiomba asitaje jina lake.
MANENO YA MAJIRANI
Kwa mujibu wa mmoja wa majirani aliyejitambulisha kwa jina la Bahati Salum, Queen alitoweka nyumbani kwao Jumapili ya Machi 12, mwaka huu ambapo mama yake mzazi aliyefahamika kwa jina moja la Lilian, akishirikiana na majirani walifanya juhudi za kumtafuta lakini bila mafanikio.
“Queen alitoweka hapa nyumbani Machi 12, mwaka huu. Nakumbuka ilikuwa majira ya saa 4 asubuhi, tulimtafuta sana hatukumpata, tulitoa taarifa Serikali za Mtaa, tukatangaza msikitini lakini hatukumpata.”
TAARIFA YAFIKA POLISI “Mwishowe, tuliamua kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha UrafikiUbungo na kupewa RB Na. UPR/RB/2091/2017
TAARIFA.
“Kesho yake kwenye majira ya jioni, tulimkuta akiwa ndani ya gari bovu ambalo lilikuwa linahamishwa kutoka gereji iliyopo hapa jirani na mwenye gari alishtuka alipomuona mtoto huyu nyuma ya siti akiwa amefariki dunia huku damu zikimtoka puani na usoni. Pia alikuwa na jeraha kwenye paji la uso kama alipondwa na kitu kizito,” alisema jirani huyo.
MASWALI YA NDUGU NA MAJIRANI
“Inauma sana! Sijui nini kilimpata mtoto huyu? Ila kinachotushangaza sisi ni kuwa na jeraha kwenye paji lake la uso. Hata kama alifariki dunia kwa kukosa hewa, damu ilitoka wapi sasa? Au inawezekana Queen aliuawa sehemu nyingine na maiti yake kufichwa pale kwenye gari? “Baada ya kuuona mwili tulikwenda kumtaarifu mwenyekiti wa mtaa ambaye aliwasiliana na Polisi wa Urafiki na kupewa RB Na. UPR/RB/2100/2017
KIFO CHA MASHAKA.
“Polisi walikuja na kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika Hospitali ya Mwananyamala (jijini Dar kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kujua kichomuua. Lakini pia, mwili wake uliharibika,” alisema jirani mwingine.
MAMA MTU APAGAWA
Kwa upande wa mama mzazi wa mtoto Queen, Lilian alipoona mwili wa mtoto wake, alijikuta akiishiwa nguvu na kupoteza fahamu ambapo, baadhi ya watu walisema ilimchukua karibu saa mbili kuzinduka. Alipokutwa na waandishi wetu, muda mwingi alikuwa akilia huku akisema anamtaka mwanaye.
“Mimi namtaka mwanangu Queen, namtaka mwanangu! Yuko wapi mwanangu Queen”
Lilian alilia kwa uchungu na kuwafanya waandishi wetu pia kutokwa machozi. Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sinza ‘D’, Muumin Herezi alikiri kutokea kwa tukio hilo pamoja na maiti ya mtoto huyo kukutwa ndani ya gari gerejini hapo ambapo ametoa ushauri kwa wazazi kuwa makini na malezi ya watoto wao.
BABU WA MAREHEMU AZUNGUMZA NA AMANI
Babu wa marehemu Queen, Frank Moshi aliliambia gazeti hili kuwa, amesikitishwa sana na kifo cha mjukuu wake na kudai familia inafanya mikakati ya mwili wa marehemu kuzikwa katika Makaburi ya Sinza.
RPC KINONDONI AZUNGUMZA Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Suzana Kaganda alikiri kupata taarifa ya tukio hilo ila kwa muda huo alikuwa kwenye kikao na hakujua nini kilikuwa kinaendelea
Inauma sana,Mungu atawalipa sawa na ukatili wao hawa waliofanya hili jambo muda.
ReplyDeleteR.I.P Queen.