Siri Vigogo Kutimuliwa CCM Yavuja...!!!!


WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimechukua maamuzi magumu katika historia ya chama hicho tangu kizaliwe kwa kuwafukuza viongozi wa juu wengi kwa wakati mmoja baada ya kubainika kukiuka misingi ya Katiba ya chama hicho, gazeti hili limebaini sababu zaidi za kufukuzwa kwa viongozi hao.

CCM juzi ilitangaza uamuzi mzito wa kuwafukuza uanachama, kuwavua uongozi na kuwapa onyo kali vigogo 22 ambao wamechangia kukihujumu na kukifanya chama hicho kinuke mbele ya jamii.

Kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), CCM imeamua kuchukua hatua hiyo ya kuadhibu viongozi wake baada ya kupokea ripoti kutoka kwa Kamati Kuu (CC) iliyokutana jana asubuhi ambayo nayo ilipokea ripoti kutoka kwenye Kamati Ndogo ya Maadili naNidhamu ya chama iliyoketi mjini hapa juzi.

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamprey Polepope ndiye aliyeutangazia umma uamuzi huo na kusema adhabu hizo zimeanza jana. Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa uamuzi huo, chanzo cha kuaminika kutoka Dodoma (jina kapuni) kililidokeza gazeti hili kuwa hatua hiyo imetokana na usaliti mkubwa uliofanywa na viongozi hao wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.

Chanzo hicho kilisema kutokana na usaliti huo, CCM ilijikuta ikipata wakati mgumu wa kukubalika katika baadhi ya maeneo kutokana na kuonekana kinanuka na kutokubalika kwa wananchi wa maeneo hayo.

Hatua hiyo mbali ya kumpunguzia kura aliyekuwa mgombea urais wake Rais John Magufuli, pia ilikifanya chama hicho kupoteza nafasi nyingine mbalimbali ikiwemo ubunge na udiwani.

Usahihi wa taarifa hizo ulithibitishwa wakati wa mkutano wa Polepole na waandishi wa habari ambapo Katibu huyo wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM alisema; “Ukiona mwanachama amefukuzwa ndani ya chama maana yake amefanya kosa kubwa.

“Mtu huyo atakuwa amefanya kitendo cha usaliti kilichosababisha chama kunuka au chama kushindwa na wanaCCM kumuona si mwenzetu na hakubaliki tena.” Waliofukuzwa uanachama Polepole aliwataja wenyeviti wa mikoa waliofukuzwa uanachama kuwa ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu, Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida, Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga, Erasto Kwilasa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara, Christopher Sanya.

Alisema katika kundi hilo la waliofukuzwa pia wamo Wajumbe wa NEC (Mnec) wa Wilaya ya Babati Ally Khera Sumaye na Wilaya ya Arumeru Mathias Manga. Wengine ni wenyeviti wa wilaya, ambapo lungu hilo limetua kwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Arusha Wilfred Ole Soilel Molel, Mwenyekiti wa Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge, Mwenyekiti wa Wilaya ya Longido Makolo Laizer, Mwenyekiti wa Wilaya ya Babati Ally Msuya na Mwenyekiti wa Wilaya ya Gairo Omar Awadh.

Wengine waliokumbwa na adhabu hiyo kubwa na ya juu kabisa kwa CCM ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake (UWT) Taifa na Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Simba. Kutokana na tukio hilo Simba pia amepoteza sifa ya kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia jumuiya hiyo.

Hata hivyo siku chache zilizopita mwana CCM huyo alitangaza nia yake ya kutogombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi wa chama hicho unaotarajiwa kuanza hivi karibuni na kumalizika ifikapo Desemba mwaka huu.

Hata hivyo katika historia CCM imewahi kuwafukuza uanachama viongozi wa juu zaidi katika uongozi kama ilivyowahi kufanywa mwaka 1988, pale ilipomfukuza Maalim Seif Shariff Hamad akiwa Waziri Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.Miaka 10 baadaye yaani mwaka 1998 ilimfukuza uanachama Hamad Rashid Mohammed.

Waliovuliwa nafasi za uongozi, kuonywa Adhabu hiyo ya NEC ya CCM haikushia hapo kwani chama hicho kilitangaza kuwavua nafasi za uongozi baadhi ya viongozi wake kwa makosa hayo ya kukiuka misingi ya Katiba ya chama hicho.

Wajumbe waliovuliwa uongozi ni Mnec kutoka Wilaya ya Tunduru Ajili Kalolo, Mnec wa Wilaya ya Singida Mjini Hassan Mazala na Mnec wa Wilaya ya Kibaha Mjini Valerian Burreta.

Aidha chama hicho kimetoa onyo kali kwa viongozi wengine ambapo waliokumbana na onyo hilo na ambao watakuwa kwenye uangalizi kwa muda wa miezi 30 ni pamoja na Mnec kutoka Wilaya ya Kilwa, Ali Mchumo.

Wengine ni Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kigoma na Mbunge wa Viti Maalum, Josephine Gezabuke, Mwenyekiti wa Wilaya ya Muleba Muhaji Bushakonyo, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Iringa Mjini Abeid Kiponza na wa Wilaya ya Singida Mjini Hamisi Nguli.

Aidha katika kuonesha kuwa haikufanya mzaha katika kufikia uamuzi huo, CCM pia imetoa adhabu kwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Balozi Emmanuel Nchimbi ambaye amepewa onyo kali na kutakiwa kuomba radhi mara moja, huku mjumbe mwingine wa Kamati Kuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Adam Kimbisa akisamehewa.

Nini hatma yao Polepole akizungumzia hatma ya waliopewa adhabu hiyo alisema pamoja na kwamba wamezuiwa kukata rufaa kupinga uamuzi huo wa NEC, lakini bado wanayo fursa ya kuwa wanaCCM au kuwa tena viongozi baada ya kujirekebisha kwa kipindi fulani, kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.

Alisema kwa waliovuliwa madaraka au kupewa onyo watakuwa katika kipindi cha uangalizi kisichopungua muda wa miezi 30 ili kuona kama wataweza kujirekebisha huku akisema kwa waliofukuzwa wanaruhusiwa kuomba tena uanachama wa CCM baada ya kupita miaka minne au miezi 48.

“Kwa hali hiyo hawa walioonywa au kuvuliwa madaraka wanakosa haki ya kushiriki katika uchaguzi wa ndani ya chama utakaofanyika kuanzia mwishoni mwa Machi hadi mwanzoni mwa Desemba mwaka huu na uchaguzi mwingine katika kipindi cha adhabu,” alisema Polepole.

Zanzibar yaundiwa Kamati Akizungumzia hali ilivyo kwa upande wa Zanzibar, Polepole alisema Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula ataongoza kamati kwenda Zanzabar kuchunguza mwenendo wa chama, uchaguzi na maadili ya wanachama.

Alisema kamati hiyo itakuwa na wajumbe Pandu Amri Kificho, Shamsi Vuai Nahodha, Maua Daftari, Daud Issa, Suleiman Saharani, Steven Wasira, Hadija na Zakhia Meghji. Alisema kamati hiyo itafanya kazi ya kuchunguza hali ya kisiasa, uchaguzi ulivyofanyika Zanzibar na maadili ya wanachama katika kisiwa hiyo, na kwamba taarifa yake itatolewa baadaye.

Ushiriki Mkutano Mkuu Polepole alisema viongozi ambao chama kimewafukuza uanachama, hawataruhusiwa kuingia kwenye mkutano mkuu wa leo, isipokuwa chama kitawapa malazi, chakula na eneo la kulala na kutakiwa kurudi makwao.

“Kwa vile CCM ni chama kinachotambua utu na kuzingatia haki, wajumbe hawa watapatiwa sehemu ya kulala, chakula na haki zao nyingine na kesho (leo) watatakiwa kurudi makwao. “

Tayari viongozi hao ambao walikuwa wakimiliki mali za chama, wahusika wameshawatembelea na kuwajulisha kwamba wanatakiwa kuziacha na kuondoka,” alisema. Polepole alisisitiza kuwa CCM imechukua uamuzi huo wa kihistoria wa kuwaadhibu viongozi wake, kama sehemu ya mkakati wake wa kufanya mabadiliko na kuwa chama cha wanachama zaidi.

Magufuli asisitiza mabadiliko Awali akifungua mkutano wa NEC, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Magufuli aliwataka wajumbe wa NEC kukubali mabadiliko yanayofanywa na chama hicho yakiwamo ya kupunguza wajumbe wake 200 kati ya 358 na kubaki wajumbe 158.

Rais Magufuli alisisitiza kwamba wanachama wanatakiwa kukubali mageuzi yanayofanyika ndani ya chama hicho ili kukiletea chama hicho mageuzi ya kweli. “Katika mageuzi haya kuna viongozi na wajumbe wa mkutano watapunguzwa wakiwamo makatibu wa CCM katika ngazi mbalimbali zikiwamo za wilaya na mikoa ambao si lazima wawe wajumbe wa mkutano wa NEC.

“Watu wanasema lazima Makatibu wa CCM Mkoa wawe wajumbe wa mkutano wa NEC, mimi nasema si lazima kama wanataka kuwa wajumbe waende wakagombee uenyekiti,” alisema.

Huku akishangiliwa na baadhi ya wajumbe, Magufuli alisema, kama suala la uwakilishi wa makatibu si lazima, kutokana na ukweli kwamba mwaka jana, wakati Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete akiingia ukumbini waliimba kwamba wana imani na mtu mwingine badala ya Mwenyekiti anayewalipa mshahara.

Mwenyekiti akauliza, kwanini makatibu ambao ni waajiriwa hawakusimama na kupigana au kupinga kitendo cha kuimba kwamba watu wana imani na mtu mwingine wala si Mwenyekiti wao wakati ndiye anayewalipa mshahara.

Magufuli alisisitiza kwamba kama makatibu wanataka kuwa wajumbe, wasuburi wakagombee katika nafasi mbalimbali zikiwamo za uenyekiti, lakini kwa sasa si lazima kuwa wajumbe.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad