Siri ya Ushindi wa Lissu TLS Yaanikwa..Lowassa Ampa Neno Hili Baada ya Kutangazwa Mshindi..!!!


WAKILI machachari, Tundu Lissu, amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) baada ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliofanyika mkoani hapa jana.

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), sasa ataiongoza TLS kwa muda wa mwaka mmoja.

Ushindi wa Lissu unatajwa kuchagizwa na mambo mengi, huku makubwa kati ya hayo yakitajwa kuwa ni kauli ya Rais Dk. John Magufuli aliyoitoa Februari 2, mwaka huu akiwa katika maadhimisho ya Siku ya Sheria, Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, pale aliposema TLS imeshakuwa kama chama cha siasa baada ya kupata taarifa ya kuwapo kwa mgombea wa nafasi ya urais ambaye ni mwanasiasa na kutokana na hilo hawezi kuwateua majaji kutoka ndani ya chama hicho.

Kutokana na kauli hiyo, Lissu aliibuka na kusema hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya msingi iliyomsukuma kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo.

Jambo jingine linalotajwa, ni kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, aliyoitoa Februari 15, mwaka huu mjini Dodoma, pale aliposema kwamba Serikali haiwezi kuona TLS inajiingiza katika siasa na kama watataka hivyo, hatosita kuifuta Sheria ya TLS sura ya 307 iliyosababisha kuanzishwa kwa chama hicho.

Dk. Mwakyembe alitoa kauli hiyo mjini Dodoma alipozungumza na wanachama wa TLS wakiongozwa na aliyekuwa Rais wao, John Seka, walipomtembelea ofisini kwake.

Alisema kitendo cha kuwaingiza wanachama wanasiasa au viongozi wa vyama vya siasa ni kuruhusu mgongano wa masilahi.

Jambo jingine linalotajwa ni kitendo cha Lissu kukamatwa Februari 6, mwaka huu mjini Dodoma akiwa anahudhuria vikao vya Bunge kwa maagizo ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na ilidaiwa alikamatwa ili achelewe kuchukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi hiyo.

Kitendo cha mawakili Godfrey Wasonga na Onesmo Mpinzile ambao ni wanachama wa TLS, kufungua kesi Dar es Salaam na Dodoma wakipinga uchaguzi huo, ambazo hata hivyo zilitupwa ni sababu nyingine inayotajwa kuchangia ushindi wa Lissu.

Si hilo tu, pia jambo jingine linalotajwa kusababisha ushindi wake ni kitendo cha Lissu kukamatwa Machi 16, mwaka huu nyumbani kwake mjini Dodoma akiwa anajiandaa kwenda Arusha na kusafirishwa hadi Dar es Salaam kwa kosa la kutotii sheria na juzi kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alikosomewa mashitaka matano ikiwamo kutoa maneno ya uchochezi yenye hisia za kidini.

Lissu alifikishwa mahakamani hapo, ikiwa ni siku moja kabla ya uchaguzi huo kufanyika jana na kulikuwa na taarifa kwamba pengine asingeweza kushiriki, lakini baadaye taarifa zilisema taratibu na kanuni za TLS zinaruhusu mgombea kuchaguliwa hata kama hatokuwapo katika ukumbi wa kupigia kura.      

Baada ya kuachiwa kwa dhamana Lissu alisafiri kwa ndege ya kukodi na kuwasili Arusha jioni na kwenda moja kwa moja Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) ambako alisababisha wajumbe wa mkutano huo kulipuka kwa shangwe wakimshangilia huku wakimwita ‘jembe’, hali iliyomlazimu Seka kuwatuliza kwa kuwaambia kitendo hicho kitawakatisha tamaa wagombea wengine.



MATOKEO YA UCHAGUZI

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo katika Ukumbi wa Simba uliopo AICC, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Dk. Kibuta Omung’wana, alisema idadi ya wajumbe waliojisajili walikuwa 3,556 na kati yao waliohudhuria ni 2,560 huku waliopiga kura ni 1,682 – zaidi ya nusu ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo.

Kwa mujibu wa Dk. Omung’wana, nafasi ya urais iligombewa na wajumbe watano ambao ni Victoria Mandari, Godwin Mwaipongo, Fransis Stolla, Lawrence Masha na Lissu.

Licha jina la Masha kujitokeza katika karatasi ya wagombea. lakini wajumbe hawakumpigia kura baada ya kujitoa wakati akiomba kura.

“Naomba nianze kutangaza matokeo nafasi ya rais, Mwapongo amepata kura 23, Mandari amepata kura 176, Stola amepata kura 64 na Lissu amepata kura 1,411.

“Hivyo namtangaza Lissu kuwa ndiye mshindi katika nafasi ya Rais wa TLS,” alisema Dk. Omung’wana.

Pia alisema mshindi wa nafasi ya Makamu wa Rais ni Godwin Ngwilimi aliyepata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanesco kabla kufukuzwa baada ya yeye mwenyewe kudai kupinga sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow. Alipata kura 1,269 na Wakili Mary Mwasongwe kura 414.

Wajumbe waliochaguliwa ni Lambaji Madai, Jeremia Mtobesi, Aisha Sinda, Steven Aweso, Husein Mtobwa, Goodluck Walter na Madeline Kimei.

MWELEKEO MPYA TLS

Akizungumza baada ya kuapishwa, Lissu alisema chini ya uongozi wake itakuwa ni mwisho kwa chombo au mtu yeyote kukitishia chama hicho.

“Ni sisi wenyewe tulioruhusu Serikali ituingilie, iwe ni mwisho. hivyo tuanze mwanzo mpya na turuhusu siku mpya ije.

 “Iwe mwisho sasa kwa chama hiki kutishwa na mtu au chombo chochote, iwe mwisho kwa mawakili kutishwa na kukamatwa ovyo, iwe mwisho kwa mahakimu na majaji kupokea maelekezo.

“Mimi ni mwanachama wa Chadema ni kiongozi, ni mbunge, ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzai Bungeni, nawahakikishia sitaileta Chadema ndani ya TLS na sitaipeleka TLS ndani ya Chadema.

“Sijagombea kama mwanachama wa Chadema bali nimegombea kama mwanachama wa TLS aliye ndani ya Chadema,” alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.

Akizungumzia uchaguzi huo, Wakili James Marenga, alisema umefanyika kwa uhuru, haki, uwazi na kwa kutumia kanuni zote za uchaguzi wa TLS za mwaka 2016.

Marenga alisema uchaguzi huo umeonyesha ni jinsi gani mawakili wanataka kuona mabadiliko ndani ya TLS itakayokuwa na uwezo wa kutoa maoni juu ya utawala wa sheria na masuala ya haki za binadamu.

LOWASSA

 Naye Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, amempongeza Lissu kwa ushindi mkubwa alioupata.

Lowassa alisema ushindi wa Lissu ni joto la moto mkubwa wa mabadiliko uliotuama ndani ya mioyo ya Watanzania.

 “Uchaguzi ule naweza kusema ulikuwa kama kura ya maoni kwa wanasheria dhidi ya Serikali jinsi inavyoheshimu demokrasia ya umma na utawala wa sheria,’’ alisema Lowassa.

PROFESA MKUMBO

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo, akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa simu jana, alimpongeza Lissu kwa kushinda nafasi hiyo na alisisitiza kuwa ushindi wake umechangiwa na Serikali iliyokuwa ikimfanyia kampeni.

 “Ushindi wake ulitarajiwa, ulifanyiwa kampeni na Serikali, tunampongeza na tunawapongeza wanasheria kwa weledi katika kusimamia taaluma na kuonyesha wanaweza kufanya uamuzi wao binafsi bila kujali mashinikizo ya viongozi,” alisema Profesa Mkumbo.

Pia alisema wanasheria wameonyesha utashi wa kitaaluma jambo ambalo ni la kishujaa na endapo  matokeo yangempa ushindi mtu tofauti na Lissu yangeleta  picha mbaya katika jamii.

RIPOTI YA FEDHA

Pia mkutano huo umetishia kuuburuza mahakamani uongozi unaomaliza muda wake kutokana na kunusa harufu ya ufisadi wa Sh milioni 78 za ada na Sh milioni 34 zilizokosa viambatanisho katika taarifa ya fedha ya mwaka 2015/2016.

Kutokana na kuibuka kwa mjadala mzito juu ya fedha hizo kwa zaidi ya saa tatu bila kufikia makubaliano, ndipo waliamua kuunda kamati ya watu watano itakayoshirikiana na uongozi mpya kuchunguza tuhuma za ufisadi huo.

Katika mkutano huo uliokuwa ukiongozwa na Seka, uliwasukuma wajumbe kutoa hoja mbalimbali zilizolenga kujua juu ya fedha zao wanazochanga kupitia ada za uanachama, baada ya taarifa hiyo kuwasilishwa mbele yao huku ikiwa imeonyesha makosa ya kiuhasibu.

Wajumbe watano wa kamati itakayoshughulikia kuchunguza tuhuma hizo ikishirikiana na uongozi mpya inaudwa na Rweikiza Rweikama, Lawrance Masha, Nicholaus Duhia, Magdalena Sylvester na Ana Julia.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad