Soma kwa Makini Hii Kitu Itakusaidia...!!!


HAKUNA anayebisha kwamba ndoa ni jambo la msingi sana katika maisha ya kila binadamu. Aidha, kuoa ama kuolewa ni heshima katika jamii na ndiyo maana leo hii wapo wanaofanya kadiri wawezavyo kuhakikisha wanapata watu wa kuwa nao kama mwili mmoja pale wanapofikia umri wa kufanya hivyo.

Kufunga ndoa kuna wakati wake, siyo kwamba pale unapojisikia kufanya hivyo basi ufanye hata kama mazingira, umri na hali yako kimaisha havikuruhusu. Lakini sasa, kibaya ambacho nimekuwa nikikishuhudia katika jamii yetu kila siku ni kwamba wapo ambao huchukulia kuoa ama kuolewa kama ‘fasheni’, hali ambayo huwasababishia kuingia katika matatizo ambayo hawakuyatarajia.

Ieleweke kwamba hadi kufikia hatua ya kutamka kwamba unataka kufunga ndoa ni lazima uwe umefanya uchunguzi wa hali ya juu na kuhakikisha kwamba unaingia katika maisha ambayo hutajutia. Suala la kuoana si la kukurupuka, ni lazima kwanza uangalie, je ni kweli unastahili kuoa ama kuolewa kwa wakati huo? Hili ni swali la msingi kujiuliza na kama jibu litakuja akilini mwako kwamba muda bado, basi unatakiwa kusubiri. Suala la kuoa ama kuolewa ni la heri na halitakiwi kuharakishwa eti kwa kufuata mkumbo. Kumbuka waswahili wanasema, mambo mazuri hayataki haraka.

Kwako wewe mwanamke, unapodhani umefikia umri wa kuolewa, kwanza unatakiwa kuangalia mwanaume sahihi, ambaye hata utakapoingia kwenye maisha hayo ya ndoa, utadumu na kufurahia. Epuka sana wanaume walaghai ambao mara nyingi hutumia gia za kuoa ili wakubaliwe kimapenzi.

Anapokutokea mwanaume na kukuambia anakupenda na angependa kuwa wako wa maisha, mchunguze kwa muda mrefu kabla hujafanya maamuzi sahihi. Usimkubalie haraka ili nawe uitwe mke wa mtu kama ilivyo kwa rafiki au ndugu yako aliyeolewa hivi karibuni. Kwa ujumla ni kwamba kabla ya kumtamkia yule ambaye ungependa umuite mke na yeye akuite mume ni lazima kwanza mtaanza kuwa wapenzi wa kawaida kisha baada ya kuona kwamba, mmependezana kitabia ndipo mtafikia hatua moja kati yenu kugusia suala la kuoana.

Kama mtaafikiana katika hilo, mnaweza kuingia katika hatua nyingine ambayo ni kwenda kutambulishana kwa wazazi wenu na baada ya hapo mtakuwa ni wachumba ambao mnatarajia kufunga pingu za maisha.

Jambo la msingi ni kuwa makini sana na nyendo za mpenzi wako katika maisha yenu ya kila siku. Mchunguze kwa undani, je anafaa kuwa mke ama mume wako? Anakufaa au umedondoka katika penzi ambalo siyo sahihi? Isije ikatokea eti kwa sababu mmekuwa wapenzi kwa muda mrefu basi atakapokutamkia kwamba anataka kukuoa, basi ukubali tu hata kama umeona kwamba maisha ya ndoa yenu yanaweza kutokuwa ya amani kutokana na kuwepo kwa migongano ya mara kwa mara pindi mlipokuwa wapenzi wa kawaida.

Wapo wapenzi ambao wanaonekana hata wakija kuoana watakuwa na maisha mazuri. Ni dhahiri kwamba wapenzi ambao wamekaa kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja na haijawahi kutokea wamegombana, kutukanana, kuvunjiana heshima kwa namna moja ama nyingine, hawa wanaweza kuoana na wakaishi maisha ya raha mustarehe.

Nimalizie kwa kusema waswahili wanasema nyota njema huonekana asubuhi na kikubwa zaidi unatakiwa kuwa na imani. Amini kwamba huyo uliyempata ambaye unataka awe mwandani wako ndivyo alivyo na ndivyo atakavyokuwa hata mtakapokuja kuoana. Usiwe na mawazo kwamba anaweza kuja kukugeuka ilimradi tu uwe umempenda na umethibitisha na yeye anakupenda.

Amini ni wako na mnastahili kuwa mke na mume na maisha ya furaha na amani yatakuwa upande wenu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad