Anaandika Wakili Msomi Tundu Lissu:
Waheshimiwa mawakili na wananchi wa nchi yetu. Nimesoma taarifa katika magazeti kadhaa ya leo kwamba Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison George Mwakyembe amenizuia kugombea nafasi ya Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS). Kama taarifa hizo ni za kweli basi naomba kuweka masuala yafuatayo wazi:
(1) Waziri wa Sheria na Katiba hana mamlaka yoyote, kwa mujibu wa Sheria iliyoanzisha TLS na kanuni zake, ya kuzuia ama kuruhusu mwanachama yeyote wa TLS kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya TLS. Hivyo, kama kweli Dkt. Mwakyembe ametoa kauli hiyo, basi huo utakuwa uthibitisho wa ama upungufu mkubwa wa uelewa wa Sheria au hulka ya ukiukaji wa sheria (culture of impunity) ambayo imeshamiri sana katika utawala huu wa sasa.
(2) Mamlaka pekee inayohusika na uchaguzi wa TLS ni Kamati ya Uteuzi (Nominations Committee) ambayo ilikwishafanya uteuzi wa wagombea wote kwa kuzingatia sifa na vigezo vilivyowekwa na Sheria na Kanuni za Uchaguzi za TLS. Mimi ni miongoni mwa wagombea ambao Kamati ya Uteuzi ilithibitisha kuwa na sifa na vigezo vya kuteuliwa kugombea nafasi ya Rais wa TLS. Kamati ya Uteuzi haijabadilisha na wala haiwezi tena kutengua uteuzi uliokwishafanyika kwa sababu za kisiasa kama za Dkt. Mwakyembe.
(3) TLS ni taasisi huru ya kitaaluma inayojitegemea na inayojiendesha yenyewe kwa mujibu wa Sheria na kanuni zake. TLS sio idara ya serikali au taasisi iliyoko chini ya mamlaka ya serikali au ya Waziri wa Katiba na Sheria au inayoitegemea serikali kwa namna yoyote ile katika kuendesha mambo yake. Uhuru huo wa TLS unatambuliwa na Sheria za Tanzania na mikataba wa kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama wake.
(4) Kwa vile mimi ni mgombea halali wa nafasi ya Rais wa TLS katika uchaguzi wa wiki ijayo, kwa sasa ninaendelea na kampeni za uchaguzi na nitaenda Arusha wiki ijayo kwa ajili hiyo.
(5) Kwa haya ya Dkt. Mwakyembe na kwa mengine ambayo yamejitokeza katika TLS siku za karibuni na ukimya wa wagombea wenzangu kuhusu masuala haya, ni wazi kwamba mimi ni mgombea pekee anayesimamia uhuru, heshima na hadhi ya TLS kama taasisi huru ya kitaaluma ya wanasheria katika uchaguzi huu. Mimi ni mgombea pekee anayeweza kuirudisha TLS katika misingi halisi ya kuanzishwa kwake na ya uwepo wake: kusimamia maslahi ya kitaaluma ya mawakili na kusimamia na kutetea utawala wa sheria. Mimi ni mgombea pekee ninayeweza kutetea maslahi ya mawakili kwa sababu sihitaji kuteuliwa na Rais kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Nawaombeni mniunge mkono kwa kunipa kura zenu mnamo siku ya uchaguzi tarehe 18 ijayo.
Source:Henry Kilewo