Tundu Lissu Apanga Kugoma Kula Mahabusu

“Nimekamatwa asubuhi na mapema. Hakuna sababu ya kutokunipeleka mahakamani leo. Kama hawatanipeleka mahakamani, nitaanza mgomo wa kula chakula, sitakula hadi nitakapopelekwa mahakamani,” amesema.

TUNDU Lissu, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amekamatwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam leo ikiwa ni dakika chache baada ya kufutiwa mashtaka ya uchochezi yaliyokuwa yakimkabili,

Lissu amekamatwa akiwa ndani ya Mahakama ya Kisutu ambapo hii leo mahakama hiyo ilitoa uamuzi wa kufuta kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili baada ya serikali kuwasilisha taarifa kuwa haina nia ya kuendelea na kesi hiyo.

“Nimekamatiwa Mahakamani Kisutu. Sikutoka hata nje ya mahakama nikakamatwa tena. Wamenipeleka Central kwa mahojiano, polisi walionikamata wamekataa kuniambia wananikamata kwa kosa gani,” amesema Lissu katika taarifa aliyoandika na kusambaza akiwa mikononi mwa polisi.

Lissu amedai kuwa, anaamini kukamatwa kwake kuna uhusiano wa moja kwa moja uchaguzi ujao wa Chama cha Mawakili hapa nchini (TLS), unaotarajia kufanyika wiki mbili zijazo.

“Serikali hii, kwa kutumia mawakili wao vibaraka, imekuwa na mkakati mkubwa wa kunizuia kugombea urais wa TLS. Walipanga kwenda kupinga kugombea kwangu mahakamani. Tumewasema hadharani na kuzianika njama zao. Sasa wameamua kutumia rungu lao la siku zote.

“Hofu yao ni kubwa sana. Natabiri watataka kuniweka ndani hadi baada ya uchaguzi huo. Mawakili vibaraka wao wataleta hoja kwenye TLS kwamba mgombea asiyekuwapo ukumbini wakati wa Uchaguzi aondolewe kwenye kinyang’anyiro hicho,” ameandika.

Lissu ameeleza kuwa hakuna makatazo yoyote katika kanuni za uchaguzi yanayozuia mgombea kuondolewa kwenye uchaguzi kwasababu tu hayupo ukumbini na amewataka mawakili washikilie msimamo kwamba wote walioteuliwa kugombea wapigiwe kura.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad