Tundu Lissu, Masha Wataka Kujumuishwa Kesi ya Kupinga Uchaguzi TLS

Wanasheria wawili wa jijini Dar es Salaam, Tundu Lissu na Lawrence Masha wamesema wataiomba mahakama kuwajumuisha kama wadaiwa katika kesi za kupinga uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) walizodai zimefunguliwa jijini Dar es Salaam na Dodoma.

Lissu, ambaye ni mbunge wa Iramba na mwanasheria wa Chadema, na Masha (mwanachama wa Chadema na waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani) wamedai kuwa kesi hizo mbili zimefunguliwa Mahakama Kuu na Godfrey Wasonga mjini Dodoma na Onesmo Mpinzile jijini Dar es Salaam, wakitaka uchaguzi huo uzuiliwe.

Mawakili hao wamewahi kupambana katika kesi mbili tofauti zilizohusu vyama vya CCM na Chadema.

Wasonga aliwahi kupambana na Lissu katika kesi iliyofunguliwa na wanachama wawili wa CCM mjini Dodoma waliopinga ushindi wa mbunge huyo wa Singida Mashariki katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, wakati Mpinzile alipambana na mwanasheria huyo wa Chadema aliyekuwa akimtetea mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali ambaye amehukumiwa miezi sita jela.

Hata hivyo, Wasonga alisema jana kuwa hajafungua kesi ila anakusudia kufanya hivyo.

Hatua ya Lissu, ambaye ni mwanasheria mkuu wa Chadema, kuchukua fomu ya kuwania urais wa TLS akisema imechagizwa na kauli ya Rais John Magufuli dhidi ya mawakili, ilibadili upepo wa uchaguzi huo na kumlazimu Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe kuuzungumzia akisema Serikali haitavumilia kuona chama hicho kinajiingiza katika siasa.

TLS imekuwa ikafanya uchaguzi kila mwaka, lakini umekuwa hauna harakati kubwa kama ulivyo wa mwaka huu. Tayari TLS imepitisha wagombea urais, wakiwamo Lissu na Masha.

Mbali na kuwa mawakili, Masha na Lissu, ambao wote wanawania urais, ni wanachama wa Chadema, jambo linaloonekana kuchochea mjadala wa siasa kuingia katika chama hicho.

Lakini, mgombea mwingine, Godwin Mussa Mwapongo, pia ni kada wa CCM aliyechukua fomu za kuwania kupitishwa na chama hicho kugombea urais mwaka 2015 ingawa hakufanikiwa. Mgombea mwingine ni Victoria Mandari.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Lissu alisema wamepata wasiwasi kuwa huenda kukawa na njama za washtakiwa katika kesi hiyo, ambao ni TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kutojitetea vya kutosha na hivyo kukubali mashtaka ili uchaguzi huo uzuiwe.

Alisema ili hali hiyo isijitokeze, wataiomba masjala ya Mahakama Kuu iliyopo Dar es Salaam, iwaunganishe katika kesi hizo kama wadaiwa.

“Uchaguzi ukizuiwa, maslahi yetu sisi tunaogombea yatakuwa yamevurugwa kwelikweli. Kwa sababu hiyo na kwa mujibu wa taratibu zinazoruhusiwa kisheria, sisi ambao tunagombea na wapigakura wanaotaka, tutapeleka maombi haraka ili tuunganishwe kwenye kesi zile kama wadaiwa,” alisema Lissu.

“Tutanunua ile kesi, kusije kukawa na njama za uongozi wa sasa wa TLS kuendelea kuongoza baada ya muda wao wa kikatiba kuisha na kusije kukawa na njama ya kuzuia uchaguzi na wale ambao wanataka kuvuruga TLS wakafanikiwa.”

Lissu alisema lengo jingine ni kutaka masuala ya uchaguzi huo yasije yakaamuliwa nyuma ya migongo yao au juu ya vichwa vyao na hivyo wanataka kupata fursa kamili ya kuiambia mahakama kwanini maombi hayo ya kuzuia uchaguzi hayana msingi wowote.

Aliongeza kuwa mawakili hao walioamua kuweka mapingamizi ni wanachama wa TLS na walikuwa na nafasi ya kuweka mapingamizi baada ya kamati ya uteuzi kutangaza majina ya wagombea.

“Kulikuwa na kipindi cha karibu wiki mbili cha kuweka mapingamizi dhidi ya wagombea walioteuliwa, fursa hiyo mwisho wake ilikuwa Machi 15 mwaka huu, lakini hakuna hata mmoja wao aliyeweka mapingamizi hayo. Itabidi tuwahoji,” alisema.

Kwa upande wake, Masha alisema hakuna mtu hata mmoja kati ya wagombea wote wa urais aliyeamua kuingia na kugombea kwa sababu za kisiasa.

Masha alisema licha ya kuwa hana nafasi ya uongozi Chadema, ni mwanachama aliyekuwa wa kwanza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais kabla Lissu hajachukua fomu hiyo.

Alisema kama kungekuwa na mbinu za kisiasa, yeye na Lissu wasingechukua fomu ya kuwania nafasi moja.

“Lissu alikuja kuchukua fomu baada ya muda wa kushiriki katika uchukuaji wa fomu kuongezwa, kama tungekuwa na njama ya kisiasa isingekuwa rahisi kwa Lissu na mimi wote kuchukua fomu kugombea nafasi moja,” alisema waziri huyo wa mambo ya ndani wa Serikali ya Awamu ya Nne.

Masha alisema chama hicho kinaongozwa kwa mujibu wa sheria na kwamba hakina uhusiano wowote katika masuala ya kisiasa.

Kuhusu matukio yaliyojitokeza Lissu alisema anashangaa kuona Serikali inaingilia suala la uchaguzi wa TLS, akisema hii ni mara ya kwanza tangu kuundwa kwake, zaidi ya miaka 60 iliyopita.

“Ni mara ya kwanza kwa Serikali kuingia moja kwa moja katika suala la nani anapaswa kuwa kiongozi wa chama hiki. Hii haijawahi kutokea tangu TLS ilipoanzishwa 1954,” alisema.

Alisema chama hicho kinaongozwa kwa mujibu wa sheria na kwamba kuwa wanachama au viongozi wa vyama vya siasa, hakuna maana yoyote ile TLS.

“Linapokuja suala la uchaguzi wa TLS nafasi zangu zote nilizonazo hazina maana. Kitu pekee chenye maana ni je wewe ni wakili mwenye sifa zote zinazotakiwa ili kuweza kugombea nafasi unayotaka kugombea katika chama cha mawakili,” alisema Lissu.

“Nadhani Dk Mwakyembe anayafahamu haya, kama atakuwa hayafahamu ni bahati mbaya sana. Wapiga kura ndio waamuzi wa mwisho kwenye uchaguzi huu. Hatutaki baraka za yeyote.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad