Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, ametoa wito wa kupunguzwa kwa mishahara ya wabunge na maafisa wakuu akisema viwango vya juu vya mishahara vimesababisha migomo ya wafanyakazi wa sekta nyingine kutaka nyongeza za mishahara.
Rais Kenyatta ameyasema hayo alipohutubia kwenye kikao cha pamoja cha Bunge la Taifa na Baraza la Senate katika hotuba yake ya mwisho ya kipindi chake cha kwanza uongozini.
Hotuba ya Rais huyo imesheheni majibu ya maswali yanayoulizwa na upinzani kila siku kuanzia ufisadi, ufujaji wa fedha za umma, kuzorota kwa huduma za afya, elimu na usalama.
Rais Uhuru amejivunia kupungua kwa visa vya mashambulizi ya kigaidi nchini, kuongezwa kwa idadi ya maafisa wa usalama na ukuaji wa uchumi ambao amesema umekuwa juu ya kiwango cha makadirio ya taasisi za kimataifa cha 3% kwa Mwaka.
Huku zikiwa zimesalia siku 145 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika Rais Kenyatta ametumia fursa ya hotuba hiyo kujipigia upatu ili aweze kuchaguliwa tena kwa kipindi cha pili.
Rais Kenyatta amesema kwamba serikali yake imejitolea kuhakikisha uchaguzi huru na haki na kuiomba Idara ya Mahakama kutotatiza matayarisho ya uchaguzi ujao.