MSANII Emanuel Elibariki ‘Nay Wa Mitego’ ameibua gumzo kubwa kufuatia kukamatwa kwake na kusafirishwa kutoka Turiani mkoani Morogoro hadi Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, kwa kile kinachodaiwa kuwa maelekezo ‘kutoka juu’ kuhusiana na wimbo wake mpya, Wapo.
Jana asubuhi, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) chini ya Katibu wake Mkuu, Godfrey Mngereza, limetoa taarifa ya kuufungia wimbo huo, wakiukataza kutumika kwa namna yoyote hadi hapo maelezo mengine yatakapotolewa.
Basata ilitoa vifungu kadhaa vinavyoipa mamlaka ya kuchukua uamuzi huo, wakisema wimbo huo ulikosa maadili.
Mchana wa jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameliagiza Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kumuachia huru Rapa Emmanue Elibariki ‘Nay wa Mitego’!
Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Rais Magufuli ametaka Nay aachiwe huru na wimbo wake uendelee kupigwa kama ulivyo katika vyombo vyote vya habari, lakini kuna baadhi ya maneno ametaka yaongezwe endapo atataka, kama wauza madawa ya kulevya na wakwepa kodi.
Rais Magufuli ameusikiliza wimbo ule kama walivyousikiliza maofisa wa Basata na mamlaka zingine. Ameona jinsi Nay wa Mitego alivyojitosa kufikisha ujumbe wake kwa namna alivyofanya.
Kuagiza kuwa wimbo huo uendelee kupigwa na kujaribu kushauri kuongeza baadhi ya mada, ni wazi Rais Magufuli hakuona popote penye ukosefu wa maadili.
Katika hali ya kawaida, hili si jambo zuri hata kidogo, hasa kwa mamlaka kama Basata, ambao wanapaswa kuona kilichoonwa na rais tokea awali.
Ukilitazama jambo hili kwa macho mawili, unabaini kuwa mamlaka zetu hazifanyi kazi zao kwa weledi, isipokuwa kwa hisia, tena za uoga. Na huenda kuna mtu anatumia ukali wa Rais Magufuli kupenyeza ajenda kwa masilahi yake, huku akiwajengea wenzake hofu.
Jeshi la Polisi lilimkamata Ney juzi saa nane usiku na baada ya kulala ‘sentro’ kwa siku moja, Basata likaupiga marufuku wimbo wake asubuhi ya Jumatatu.
Kinachotokea ni watu, hawa walio katika mamlaka, kutekeleza majukumu yao kwa uoga na kujaribu kumtafsiri kiongozi mkuu wa nchi, badala ya kuangalia sheria walizoapa kuzisimamia zinasema nini.
Hii ni hatari, Nay amefanikiwa kutoka mikononi mwa dola kwa sababu habari zake zimemfikia rais kupitia mitandao, vipi kuhusu makumi kwa mamia ya watu wasio na umaarufu wanaotupwa selo kwa staili hii Tanzania nzima?