Ukweli Mtupu..Chid Ukirudi Ulikotoka, Tutashangaa sana!


HI…chi…chii Chid Benz! Inakuwa vigumu sana kuacha kuandika kuhusu huyo mkali wa Hip Hop Bongo.

Unamtazama akiwa bado kinda anapovamia jukwaa la vijana wenye majina katika Bongo Fleva, unamuona anavyopenya na kung’ara katikati yao, lakini ghafla, unamuona akijimaliza kikatili! Nimewahi kuandika mara kadhaa katika safu hii kuhusu Rashid Makwiro na mara moja kati ya hizo, niliwahi kupata simu kutoka kwake na tukazungumza kwa muda mrefu, akinilalamikia kwamba nilikuwa na uwezo wa kumtafuta na kumkalisha chini kama mdogo wangu, nikamweleza mwenendo wake na tukaelewana, kuliko kumuandika, kwani anayo familia inayoumia kwa kuandikwa kwake.

Nilimuelewa, nikamuomba radhi kwa kumuumiza na kuahidi kuwa nitajitahidi mara nyingine nimtafute endapo atateleza na tuzungumze. Lakini Chid Benz wa kwenye simu si Chid unayekutana naye mtaani. Ni watu wawili tofauti na njia pekee ya kumfi kia kwa ufasaha ni kuendelea kuandika.

Na nina muandika siyo kwa sababu nina wivu naye, ila kwa sababu ninaumia kuona kipaji chake kikipotea bure na hasa ukizingatia kuwa siioni kazi ambayo Chid anaweza kuifanya na kuendesha maisha yake na familia zaidi ya muziki.

Kama kuna marapa ambao nchi yetu imewahi kuwapata, huyu ni mmoja wao. Alikuwa anapokea kijiti kutoka kwa kaka zake kina Profesa Jay, Sugu, Solo Thang na wenzao na yeye alikuwa na muda mwingi wa kukikimbiza. Lakini bahati mbaya sana, Chid ameingia kwenye mtego mgumu kujinasua, japo inawezekana kabisa.

Mara ya mwisho picha za msanii huyu zilizoonekana, zilimtisha kila mmoja anayemfahamu, akionekana kama mtu ambaye siku zake za kuishi zilielekea ukingoni. Mungu siyo Athumani, haijulikani msamaria mwema huyu aliibuka kutoka wapi, lakini akamkimbiza Chid Benzino mjini, akampeleka Iringa, huko Mafi nga ambako aliweza kusaidiwa na kuurejesha mwili wake katika hali yake ya kawaida.

Wiki mbili zilizopita, ilikuwa ni vigumu kidogo kuamini kama picha unayoitazama ni ya King Kong, maana ilikuwa na mabadiliko ya asilimia 100 na hapo awali. Bwana Ametenda! Hili siyo jaribio la kwanza kwa watu kutaka kumweka Chid katika mstari salama.

Wamefanya hivyo watu wake wengi wa karibu na wameshindwa. Huyu wa sasa amekaribia kwenye ukweli. Nina uzoefu na wabwia unga, nimeishi nao na wengine ni rafi ki zangu.

Baadhi wamepoteza maisha. Ukitaka ukaribu na rafi ki yako mla unga upotee, mkanye kuhusu kubwia. Hatapenda kuwa karibu yako na kila ukikutana naye, atakuambia ameacha, hata kama unamuona ‘anabembea’.

Kwa Chid, uamuzi anao mwenyewe moyoni mwake. Anapenda aendelee kuishi au hataki ni juu yake kuchagua. Yeye hawezi kuwa wa kwanza kuacha, wako wengi.

Yupo msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Terry Fanani. Hawa ndiyo watu wa kwanza kwanza kwenye game kuanza kula ngada. Ninamfahamu Fanani na ninajua kwa kiasi gani anapambana kwa zaidi ya miaka kumi sasa kuachana na jambo hili.

Yupo Msafi ri Diouf, yule rapa mkali katika Muziki wa Dansi, aliyekuwa Twanga Pepeta. Ilifi kia wakati Diouf alikuwa akibwia na kupoteza fahamu, akilala popote bila kuchagua wala kujali. Leo hii ameachana nayo, na sasa yupo zake Uingereza, akifanya shughuli zake za kumuingizia kipato. Q Chillah ‘alikula sembe’ hivi sasa ameacha.

Rai yangu kwa Chid Benz, usirudi kule ulikotoka, ukirudi nitakushangaa sana. Mimi ni shabiki namba moja wa ile sauti yako nene, yenye mamlaka, inayokwaruza, ambayo ni moja ya silaha kubwa katika muziki wako. Hivi sasa Chid alipaswa kuwa tajiri mwenye utitiri wa mali badala yake ameshindwa kupiga hatua kwa sababu ya ‘sembe’.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad