KATIKA historia yake ya miaka 50 na ushee, Tanzania haijawahi kuwa na Mke wa Rais, mstaafu au aliye madarakani, bungeni. Wiki iliyopita, Rais John Magufuli akaweka historia mpya kwa kumtangaza Salma Kikwete, mke wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, kuwa Mbunge wa Kuteuliwa.
Na Mama Salma si First Lady wa kawaida. Kwenye historia ya miaka 50 hiyohiyo, Tanzania haijawahi kuwa na mke wa Rais ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mwaka juzi, nilikuwa ndani ya ukumbi wa Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma wakati wa kinyang’anyiro cha kutafuta mgombea urais kupitia chama hicho.
Mama Salma alikuwa amekaa pembeni ya Benard Membe aliyekuwa mmoja wa wagombea waliokuwa wakipewa nafasi kubwa kushinda.
Wakati wake wa marais waliopita wa Tanzania walikuwa hawatajwi katika vinyang’anyiro vya namna hii; haikuwa siri kwamba Salma alikuwa akitaka Membe ndiye awe Rais wa Tanzania baada ya Kikwete.
Na ndiyo sababu, ilikuwa ikijulikana kuwa Membe huyohuyo ndiye alikuwa chaguo la Kikwete mwenyewe. Na hii ni kwa sababu, haingewezekana kwa Salma kupiga kampeni hadharani kwa mtu ambaye mumewe hamuungi mkono.
Mara baada ya Magufuli kumtangaza Salma kuwa mbunge, nilichora kwenye karatasi duara moja lililozungukwa na miduara mingine mingi. Lengo langu lilikuwa kutafuta sababu hasa za Rais kufanya uteuzi ambao hakuna aliyekuwa akiutarajia.
Uteuzi wa Salma unahitaji tafakuri ya kipekee. Huyu ni mwanasiasa ambaye tayari ameshiriki katika siasa za juu kabisa za taifa letu. Kama ana ndoto au mpango wowote ule, hauwezi kuwa mpango wa mambo madogo madogo.
Tafakuri yangu ilinifikisha pia katika tukio lilitokea mwishoni mwa wiki hiyohiyo; wakati Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Sofia Simba, alipotangaza kuwa hatawania tena nafasi hiyo.
Salma, anaweza kabisa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa UWT. Hii ni kwa sababu sasa anakijua chama chake vizuri, anajulikana miongoni mwa akinamama nchini na kwa sababu ya mumewe, tayari ana kada maarufu wa chama nyuma yake.
Na kama Salma atakuwa Mwenyekiti wa UWT, maana yake ni kwamba atakuja kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Ukichanganya na nafasi yake bungeni, maana yake ni kwamba atakuwa na fursa pana ya kukutana na watu na makundi mbalimbali.
Hadi sasa, mwanamke mwenye madaraka makubwa kuliko wote hapa nchini ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. Kwenye siku za karibuni, ushawishi wake katika jamii umekuwa ukiongezeka kila kukicha.
Kuna wanaoamini kwamba tayari ana sifa za kumrithi Dk. Ali Mohammed Shein kwenye uchaguzi ujao wa Zanzibar na kuna wanaoamini kwamba kama Tanzania iko tayari kwa Rais wa kwanza mwanamke, Samia yuko katika nafasi nzuri sasa kuliko mwanamke mwengine yoyote.
Ujio wa Salma kwenye siasa, unapunguza kidogo nguvu ya ushawishi wa Samia. Ni wazi kwamba Kikwete alipigiwa kura nyingi na wanawake wakati akitafuta urais na ni rahisi kwa mapenzi hayo kuhamia kwa Salma.
Pia, miaka tisa ijayo, watoto wa kike ambao walisomeshwa na Salma kupitia taasisi yake ya Wanawake na Maendeleo (Wama), watakuwa watu wazima ambao wana ushuhuda wa namna mama huyu alivyowasaidia.
Hata hawa wasanii maarufu wa kike na kiume hapa nchini ambao kwa sasa wanaonekana kumuunga mkono Samia, watahamia kwa Salma kirahisi tu kama Kikwete atataka hivyo.
Hii ni kwa sababu, hakuna kiongozi mwengine hapa nchini anayeweza kujidai kuwa na ushawishi mkubwa kwa wasanii hapa nchini kuliko Jakaya.
Kama Magufuli angeacha hali ya sasa (status quo) iendelee, ni wazi kuwa Samia ndiyo angekuwa mwanamke mwenye ushawishi mkubwa kuliko mwengine yeyote hapa nchini kuelekea 2020 na 2025.
Hadi sasa, hakuna anayejua sababu hasa za Magufuli kumteua Salma kuwa mbunge. Kwa wanaofahamu siasa za CCM zilivyo sasa, si siri pia kwamba hatua hii inaonekana kuwa na lengo la kukiweka chama pamoja.
Lakini, wakati nachora duara zangu za kuangalia nje ya boksi, nimeona pia kwamba hatua hii ya Magufuli –hata kama pengine yeye hakuwa na dhamira hiyo, inapunguza ushawishi wa kisiasa wa Makamu wake wa Rais walau kwa Tanzania Bara.
Bila shaka, kuanzia siku ambayo Salma ataapishwa rasmi kuwa mbunge, ramani mpya ya michezo ya kisiasa ndani ya CCM itaanza kuchorwa.
Na kwa kuanzia, wiki ijayo, nitaeleza namna kinyang’anyiro cha kuwania urais kumrithi Magufuli kitakavyoathiriwa na uteuzi huu wa sasa wa Mama Salma Kikwete.
Imeandikwa na Ezekieli Kamwaga wa Raia Mwema