KATONI 32,634 za pombe kali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (viroba) zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 5.18 zimekamatwa jana, katika operesheni maalumu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kusitisha uzalishaji, usambazaji, uingizaji, uuzaji na matumizi ya pombe hizo.
Pombe hizo zimekamatwa katika operesheni inayoendelea katika mikoa mitatu ya Kikodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dar es Salaam ambayo ni Temeke, Kinondoni na Ilala.
Akizungumza katika operesheni hiyo, Mkaguzi kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), John Nzila alisema walikamata katoni 14,393 za konyagi, katoni 9,964 za Vradmill, Zanzi 31 na Valeur. 268.
Alisema mzigo huo ulikutwa katika ghala la Loverira Enterprises lililopo Kimara Temboni na kwamba mzigo huo umezuiwa kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake Mwanasheria Mwandamizi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Heche Suguta alisema kuwa walikamata katoni 7,000 za viroba vya aina mbalimbali zikiwemo Konyagi, Zanzi pamoja na Burudani vyote vikiwa na thamani zaidi ya Sh bilioni 2.
Alisema vinywaji hivyo vilikutwa katika duka la Love Kira Enterprises lililopo Wazo na kwamba mzigo huo umezuiwa hadi utaratibu mwingine utakapotangazwa.
Kwa upande wa Temeke yalikamatwa maboksi matano ya Konyagi, maboksi 15 ya Black Bee, maboksi nane ya Zanzi na Maboksi matano ya Valeur.
Ofisa Afya wa Manispaa ya Temeke ambaye pia ni mratibu wa Masuala ya Chakula katika Manispaa hiyo, Rehema Sadick alisema katika operesheni hiyo wamegundua kwamba wafanyabiashara wengi hawana vibali vya TFDA na leseni za biashara.
Hata hivyo katika operesheni hiyo pia kulibainika kuna baadhi ya wafanyabiashara wanauza vileo vilivyokwisha muda wake na hivyo kuvikamata kwa ajili ya kuokoa afya za watumiaji.