Vyeti Kumng`oa Rc Makonda?


Sintofahamu! Jumapili iliyopita kwenye mahubiri ya ibada ya Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mchungaji Kiongozi, Josephat Gwajima alitoa madai mazito sana kwamba, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda (36) anatumia cheti cha kidato cha nne cha mtu anayeitwa Paul Christian Muyenge wakati yeye alianza darasa la kwanza mwaka 1988, akitumia jina la Daudi Albert Bushite.

Akihubiri huku waumini wake wakimsikiliza kwa umakini mkubwa, Mchungaji Gwajima alisema kuwa, mwaka 2001, Makonda alitumia cheti cha mwanafunzi huyo chenye divisheni 3 ya ponti 25 ili aweze kujiunga na Chuo cha Uvuvi Nyegezi (NFTI).

AMCHAMBUA KWA VYUO

Alisema kuwa, alisoma masomo ya certificate  na kuhitimu mwaka 2002 ambapo mwaka huohuo, akiendelea kutumia jina la Paul Christian Muyenge, alijiunga na Chuo Cha Uvuvi Mbegani, Bagamoyo mkoani Pwani kwa masomo ya Diploma ya Uvuvi (ODMF, NTA LEV. 6) na kuhitimu mwaka 2005.

Gwajima alizidi kusema kuwa, mwaka 2006, Makonda alipata udahili Chuo cha Ushirika na Biashara, Moshi (wakati huo kikiwa Chuo Kikuu Kishiriki cha SUA) akiendelea kutumia vyeti vyake vya certificate ya Nyegezi na diploma ya Mbegani na akijulikana kama Paul Christian Muyenge.

NI JINA LA MAHAKAMANI?

Mchungaji Gwajima alizidi kudai kuwa, jina la Paul C.  Makonda, analitumia baada ya kula kiapo mahakamani kubadili jina na kwa hiyo, cheti cha kidato cha nne cha mheshimiwa kinasomeka, Paul C. Muyenge lakini vyeti vya elimu ya juu vinasomeka Paul C. Makonda baada ya kuapa mahakamani.

Kwa mujibu wa maelezo ya Gwajima, ana maana jina la Daudi lilikufa rasmi kwenye makahama na kuanza kuchipuka kwa jina la Paul.

NANI ANAINGIA?

Kwa mujibu wa Mchungaji Gwajima, mwanafunzi aliyeuza cheti hicho (Paul Christian Muyenge) anaingia kwenye kashfa ya kuuza cheti kama kweli mtu huyo yupo na ndiye mwanafunzi halali aliyekuwa akilitumia jina hilo mpaka mwaka 2001.

MKANGANYIKO WA GWAJIMA, PAUL CHRISTIAN

Wakati Gwajima akidai kuwa na nakala za vyeti vyote viwili vya Paul Makonda, vikiwemo vile alivyotumia kuanzia kidato cha nne, upo mkanganyiko mkubwa kutokana na maelezo ya Paul Christian (mtu aliyedaiwa kumpa vyeti Makonda) aliyoyatoa kwa gazeti moja la kila siku la hapa nchini.

Paul Christian, anayedaiwa kuwa ndiye ambaye cheti chake kilitumiwa na Paul Makonda aliliambia gazeti hilo;

“Paul Makonda nimemfahamu kupitia habari na jina wanavyolitaja (waliotunga taarifa ya mtandaoni) wanakosea kwani mimi naitwa Paul Pierre Christian Kagezi, hatuna uhusiano, mimi Mhaya yeye Msukuma.”

“Taarifa hizo (za kumpa cheti Makonda) si za kweli kwa sababu huwezi kutoa cheti wakati umepata daraja la kwanza kidato cha sita, utakwenda vipi chuo kikuu? Sasa niliwezaje mimi kwenda chuo kikuu halafu kwa wakati huo nimpe naye aende chuo kikuu?”Alihoji.

Cristian aliendelea kudai kuwa katika kidato cha tano na sita, alichukua mchepuo wa sayansi masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu (PCM), hivyo si rahisi kutoa cheti hicho kwani angeshindwa kumudu huko alikokwenda.

Alihoji kama Makonda hakufanya vema kidato cha nne au hakusoma kidato cha sita, akatumia cheti cha mtu mwingine, angeweza vipi kufanya vema katika mitihani yake ya chuo kikuu?

Alifafanua kuwa watu wamekuwa wakipika na kuoanisha majina yao, huku akiendelea kukanusha kuhusu taarifa hizo.

“Kama wanataka kumpata huyo bwanamdogo (Makonda) kwa njia hiyo wamemkosa, kwani kwa mantiki nimekuuliza ukipata daraja la kwanza kidato cha sita lazima uende chuo kikuu?” alihoji.

“Huyo bwana anajitegemea yeye kama yeye na walichokifanya wao (waliosambaza taarifa mtandaoni) kwa makusudi yao bila shaka wana lengo lao, wao wametaka kuingiza hoja ambazo hazina mashiko.”

  

MKANGANYIKO (CONFUSSION) MKUBWA

Kufuatia madai hayo ya Gwajima ambayo yalikuwa ndani ya mahubiri yake, mitandao ya kijamii na mazungumzo ya watu mitaani, sehemu mbalimbali ya nchi, gumzo kuu likawa ni jina la; ‘Paul Muyenge na Daudi Bashite.’

Baadhi ya watu walionesha kushangaa kwao kama kweli Makonda anatumia cheti cha mtu mwingine huku akijua kuwa, serikali ya awamu ya tano chini ya utawala wa Rais John Pombe Magufuli ilitangaza kupambana na watumishi wenye vyeti vya bandia.

“Hivi inawezekanaje Makonda akaendelea kutumia cheti cha mtu mwingine wakati mkuu wake wa nchi ni mkali kwenye eneo hilo? Hili jambo si la kulifumbia macho kirahisi tu, ni jambo zito. Gwajima akae na kujua kuwa, alitoa tuhuma nzito sana ambazo kama zinathibitika zina ukweli, Makonda anaweza kung’oka kwenye nafasi yake” alisema Bakar Msumari, mkazi wa Mbezi Mwisho.

HOTUBA YA MAGUFULI KUHUSU VYETI FEKI

Katika moja ya hotuba zake za kuonesha mwelekeo wa serikali yake, Rais Magufuli alisema kuwa, atakapogundua, mtumishi yeyote katika serikali yake anatumia vyeti feki, basi atamfukuza mara moja bila kujali ni nani (akimaanisha hatajali cheo). Na tangu aanze utawala wake, Magufuli amekuwa ni mtu anayesimamia kile anachokiongea.

“Ndugu zangu Watanzania katika hili la vyeti wala hawana sababu ya kuwa na hofu, tunachotaka sisi ni kujua je, huyu mtu anayelipwa kwa sababu ana masters, kweli ni yake? Kwa sababu kuna watu wanalipwa mishahara mikubwa kwa sababu ya vyeti vyao ambavyo kiuhalisia siyo vya kwao. Wewe kama umeishia darasa la saba, usihofu, utaendelea na kazi kama kawaida,” alisema Magufuli akimaanisha kuwa, hataki watumishi wenye vyeti feki.

Baada ya hotuba hiyo, watumishi wa umma wenye vyeti feki walianza kusakwa kote nchini, wakiwemo wa Mkoa wa Dar es Salaam na wale ambao wamebainika, walichukuliwa hatua na zoezi bado linaendelea.

UFUMBUZI NI UPI?

Baadhi ya watu waliamini kuwa, maneno ya Gwajima si jambo la kuwafanya waamini ni kweli kutokana na historia ya mtumishi huyo wa Mungu ambapo, amewahi kukwaa kesi mahakamani kufuatia kudaiwa kumtusi Kadinali Polycarp Pengo katika ibada moja aliyoifanya kwenye kanisa lake (wakati huo, Kawe).

Wengi walisema kuwa, alichokiongea Gwajima si ukweli kwa asilimia mia moja, bali mwenye ukweli ni Makonda mwenyewe ambaye wasomaji wanaamini ndiyo mwenye uwezo wa kuanika ukweli na kufuta madai ya Gwajima na ufumbuzi wa madai yake kujulikana.

Ijumaa liliweza kuongea na baadhi ya wasomaji ambao walisema kuwa, ni wakati muafaka kabisa kwa Makonda kuibuka na kuweka wazi au kujibu tuhuma za Gwajima ili mambo yaishe na maisha yaendelee.

“Gwajima si msemaji wa mheshimiwa Makonda, aliyoyasema si kwamba ndiyo ukweli. Kwani mara ngapi watu wanaibuka na kujifanya wanawajua wengine lakini baadaye inabainika kuwa si kweli?” alisema msomaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la David Mashaka, mkazi wa Salasala, Dar.

“Nilimsikia Gwajima, lakini sijakubaliana naye moja kwa moja. Makonda ndiye mwenye ukweli wote. Ufumbuzi wake ni kwamba, Makonda ajitokeze na kuweka wazi anachokijua yeye, siyo mtu mwingine tu amsemee,” alisema Omar Kishapu, mkazi wa Kimara Suka.

FAIDA ZA MAKONDA KUTOBOA UKWELI

Baadhi ya watu wamesema kuwa, Makonda kujitokeza na kutatua fumbo hilo kutaleta faida kwani atakuwa ameilinda serikali yake ya awamu ya tano lakini pia atakuwa amemsaidia Rais Magufuli katika kukitimiza kile anachokisimamia kama rais wa nchi.

“Inawezekana Makonda kuendelea kukaa kimya kukawapa watu neno la kumsema rais kwamba mbona hamchukulii hatua. Lakini kumbe hamchukulii hatua kwa sababu anaujua ukweli, lakini je wananchi wanaujua ukweli? Si mpaka Makonda mwenyewe auseme, akiuanika ukweli itampa heshima Magufuli na yeye mwenyewe pia ataendelea kuheshimika na kuaminika,” alisema  Maria Kaparasule, mkazi wa Boko, Dar.

IJUMAA NA VIONGOZI

Juzi, Ijumaa liliwatafuta baadhi ya viongozi ili wazungumzie madai ya Gwajima ambapo, awali Msemaji wa Tume ya Maadili ya Watumishi wa Umma, Honoratus Ishengoma alisema:

“Mimi kwanza kabisa nipo likizo. Lakini madai ya Gwajima kusema ule ukweli ni mazito sana. Hayo madai yanatakiwa kusemewa na Mkurugenzi wa Tume ya Maadili.”

Ijumaa lilimpigia simu, bosi wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma lakini hakupatikana hewani mara moja.

MEYA WA KINONDONI

Ijumaa lilimpigia simu, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta ambaye Gwajima alimtaja kuwa rafiki kipenzi wa Makonda lakini simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa hata iliporudiwa tena na tena.

PROFESA SEMBOJA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja yeye alipoulizwa kuhusu madai ya Gwajima alisema:

“Kosa la Makonda ni kutaja majina ya watu na kuwatuhumu kufanya hivi wakati hawajathibitika, sasa na sisi hatupaswi kurudia makosa hayo ya kumtaja kwa jambo ambalo hatuna uhakika nalo. Ni jukumu lenu nyinyi kama waandishi wa habari kuchimbua na kuja na majibu, je, vyeti hivyo ni feki au la.

“Hapa kuna hoja mbili, ya kuwa na vyeti feki au kutumia jina la mtu katika masomo yake. Mimi ni mtu mzima, wakati wetu, lilikuwa ni jambo la kawaida mtu kusomea jina la mtu mwingine, ambaye alishindwa kuendelea na masoma kwa sababu mbalimbali. Kama alisomea jina la mtu mwingine, lakini masomo alisoma yeye, sioni kama kuna tatizo, ila kama elimu aliyonayo hajawahi kuipata darasani, hilo ndilo tatizo.

“Mimi nadhani tujikite katika kumsaidia rais kwenye mambo magumu anayofanya, kwa sababu ndiye rais anayesimamia vitu kikamilifu, tusimchoshe kwa vitu vidogovidogo, kwangu mimi Makonda ni mchapakazi, huenda ndiyo maana anakutana na vigingi, lakini kwa kweli siwezi kusema lolote hadi ithibitike kosa lake hasa ni lipi.”

TUMEFIKAJE HAPA?

Februari 2 na 9, mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alianza zoezi la kutangaza majina ya watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya ‘unga’ kwa maana ya kuuza au kutumia. Kila aliyemtaja alitakiwa kufika Kituo Kikuu cha Polisi Dar ‘Sentro’ kwa mahojiano na polisi. Miongoni mwa watu waliotajwa ni Gwajima.

Gwajima alifika kituoni hapo na kuwekwa ndani kwa siku kadhaa kisha akaachiwa. Baada ya kuachiwa, alifanya mkutano na waandishi wa habari akionesha kusikitishwa kwake kwa Makonda kumtaja jina yeye akidai kuwa, hajawahi kutumia unga wala kuuza.

Kwa hiyo kumtaja kwake kwamba anatumia vyeti feki inaweza kuwa ni katika kutoa hasira au ‘kulipa kisasi’ dhidi ya Makonda.


Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Nimependa sana analysis za professor. Usomi lzm unaonekana kwenye uelewa wa jambo. Lkn watu pia wafahamu kuwa ukuu wa mkoa hauna interview wala qualifications. Ni nafasi ya kuteuliwa. Sasa sijui hoja ya kukomaa na vyeti zinakujaje.

    ReplyDelete
    Replies
    1. katiba iko wazi kabisa kwamba ni kosa la kutumia vyeti vya mtu mwingine,kwaiyo hoja hapa ni kwann utumie vyeti vya mtu mwingine kinyume na katiba???

      Delete
  2. Unajua vitu vi gine ni virahisi lakin tunavifanya kuwa vigumu, embu jiulize, Makonda anashindwa nin kuweka vyeti vyake hadharan kukanusha yasemwayo? ukiona kunaugumu katika kwa Makonda kufanya hivyo badi ujue kuna tatizo.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad