DAR ES SALAAM: Siku nne tu baada ya watu waliotajwa kama mashehe kuingia na kuhudhuria ibada katika Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, lililopo Ubungo Maji, jijini, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Salum, amewalipua kuwa hawakuwa viongozi wa dini ya Kiislamu, bali ni watu waliovaa vazi la kanzu, ambalo kila mtu anaweza kulivaa.
Akizungumza na Amani jana, kiongozi huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Amani mkoani Dar, alisema siku zote ndege wamoja hutambuana, kama ilivyo kwa maaskofu na wapiga debe, hivyo wao kama mashehe, hawajaona mtu mwenye hadhi ya kuitwa shehe, zaidi ya kuwaona watu waliovalia kanzu na vibalaghashia.
“Hakuna shehe pale, wale ni watu tu wamevaa kanzu na vibalaghashia, siyo kila mvaa kanzu ni shehe, mtu yeyote anaweza kuvaa, kwani kanzu ni vazi kama vazi jingine na ndiyo maana zinauzwa madukani.
“Siku zote mashehe tunatambuana, hata maaskofu, wapiga debe wanatambuana, wale sisi hatuwatambui kama mashehe. “Na ndiyo maana tulitoa tamko kama Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kuwa wale hawakuwa mashehe kutoka Bakwata na wala hawakuwa na baraka za Bakwata,” alisema shehe mkuu huyo.
Mashehe wanaozungumzwa ni wale ambao walienda kanisani katika siku ambayo pia wasanii wa vichekesho, Stanley Yusuph ‘Stan Bakora’ na Musa Kitale, ‘Mkude Simba’ walihudhuria ibada kwenye kanisa hilo.
Tukio hilo lilitokea Machi 26, mwaka huu na kuzua mshangao hata kwa waumini wa kanisa hilo ambao walishindwa kujizuia na kulipuka kwa kelele za ushindi, zilizoambatana na shangwe, miluzi na vifijo.