Haya yanayotokea, marais wetu wastaafu, Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa na Alhaj Ali Hassan Mwinyi, hawayaoni?
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, enzi zake baada ya kustaafu, hakupoteza macho ya kuona wala masikio ya kusikia. Alipoona mambo hayapo sawa, alitokeza na kuzungumza.
Faida ya kuwa na wazee ni kupata busara zao katika vipindi tofauti. Hii hali na wasiwasi mkubwa uliopo, je, wao hawaoni? Mbona hawatoki na kusema chochote?
Je, hii hali iliyopo inawafurahisha wazee wetu? Siyo vibaya, watokeze hata wasifie tujue kuwa wazee wetu wanaunga mkono kinachofanywa na Rais wetu mpendwa, Dk John Magufuli.
Hali ilivyo, wananchi wamegawanyika makundi mawili, wapo wanaosema Rais anapatia, wengine wanaona anakosea. Mbona sasa wazee hawatokezi na kusema chochote?
Je, wazee wanampinga Rais Magufuli? Watoke na waseme kuwa kinachofanywa na Rais hakipo sawa. Je, ukimya huu maana yake nao wanaogopa kusema?
Kwa nini wazee wetu wanatufanya tutamani Mwalimu Nyerere afufuke? Kwa nini mnakaa kimya kama vile hamuoni hali iliyopo?
Wazee Joseph Warioba, John Malecela, Salim Ahmed Salim, Cleopa Msuya na wengine, tokezeni mseme. Hata kama ni kusifia, sifieni tu ili tujue wazee wetu wanasimamia wapi.
Je, wazee wetu wamepoteza ujasiri? Nakumbuka akina Butiku na Warioba walivyokuwa wajenzi wa hoja kinzani dhidi ya Serikali wakati wa JK, ujasiri huo umekwenda wapi?
JK upo wapi mkuu? Mkapa hutokezi baba! Mwinyi umejichimbia wapi mzee?
Mwalimu Nyerere hakuwahi kutuacha kama ambavyo ninyi mnatuacha. Ni kama baada ya kumaliza utawala wenu mmeamua kunawa mikono, hapana! Bado mnayo kazi ya kufanya. Kushauri, kukosoa, kusahihisha au kusifia.
Nchi bado inawategemea mno kwa busara na uzoefu wenu. Mwalimu Nyerere alijua kuwa Tanzania ilimhitaji ndiyo maana hata baada ya kung'atuka alibaki nasi, akawa anatokeza na kuzungumza kwa kuyajenga kuhusu nchi yetu.
JK, Mkapa na Mwinyi, kila mmoja ameongoza nchi miaka 10. Rais Magufuli ndiyo yupo mwaka wa pili. Tokezeni mseme jambo la kumshauri. Au kama huwa mnamshauri kimyakimya afanye anayofanya, basi tokezeni msifie utekelezaji wake.
Ndimi Luqman MALOTO
Kwli fimbo imewaingia,Mnahaha tu mara hili mara lile.Makonda nasema piga kazi kaka yetu jembe ziba masikio.nape wasalimie wenye tabia kama zako siyo Kwa magufuli.Hapa kazi tuuuu.tunampenda makonda hata mkimuandika vibaya sisi tunamkubaliii wakinamama wotee.mliee tu
ReplyDelete