Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeshauri Watanzania kuwa na utamaduni wa kuandika wosia wa kuchangia viungo vya binadamu wanapofariki, ikiwamo moyo.
JKCI imetoa usahuri huo baada ya kuwa katika matarajio ya kuanza upasuaji wa kupandikiza moyo mwingine nchini, kwa wagonjwa wenye matatizo ya kiungo hicho muhimu mwilini.
Mkurugenzi wa Upasuaji na daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu, Dk. Bashir Nyangasa alitoa ushauri huo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu malengo ya taasisi hiyo.
“Tuko katika maandalizi ya kuandaa mapendekezo kwa ajili ya kupeleka bungeni ili Bunge liridhie na kupitisha sheria itakayoruhusu mtu kuandika wosia wa viungo vyake kutumika baada ya kufariki, ikiwamo moyo, figo na viungo vingine,” alifafanua Dk. Nyangasa.
Alisema umefika wakati kwa Watanzania kujiwekea utaratibu wa kuacha wosia wa kutumika kwa viungo vyao baada ya kufariki.
Alisema baada ya Mtanzania kufariki, kiungo husika kitatolewa kwenye maiti na kuhifadhiwa katika benki za viungo ili viweze kutumika na watu ambao wanauhitaji.
Aidha, Dk. Nyangasa amesema hospitali ya Apolo Bangalore ya India na hospitali nyingine za kimataifa za magonjwa ya moyo, kwa sasa zimehamia JKCI kutokana na huduma pamoja na vifaa vinavyopatikana katika hospitali hizo vinapatikana katika taasisi hiyo.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Huduma za Tiba, Daktari Bingwa wa Wagonjwa wa Moyo, Dk. Tulizo Shemu amesema kwa mwaka 2016 JKCI imefanya uchunguzi wa tiba kwa wagonjwa 973, kati ya wagonjwa hao 620 walipatiwa matibabu ya moyo ya bila kufungua kifua kwa kupitia mishipa ya damu (Catheterization) na wagonjwa 353 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua.
Aidha, Dk. Shemu alisema kwa mwaka huu taasisi hiyo imejipanga kufanya upasuaji wa kupasua kifua kwa wagonjwa 700 na wagonjwa wengine 1,000 watafanyiwa operesheni bila ya kufungua kifua.
Taasisi hiyo inategemea kuwa na kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Open Heart International ya nchini Australia kuanzia keshokutwa; ambapo wagonjwa 25 wakiwamo watoto 15 na watu wazima 10 watafanyiwa upasuaji.
Wananchi wameombwa kujitokeza kuchangia damu kutokana na uhitaji wa damu nyingi katika upasuaji huo.