Mwili uliokataliwa na ndugu kuchukuliwa katika Hospitali ya KCMC baada ya kukuta umeandikwa jina la mtu mwingine hatimaye umepatiwa ufumbuzi.
Maiti huyo ambaye alibaki hospitalini hapo kwa saa 12, juzi ndugu zake walithibitisha kwamba alikuwa ni ndugu yao baada ya picha iliyopigwa na kutumwa kwenye mtandao wa WhatsApp kusaidia kutambuliwa.
Ndugu hao waliichukua maiti hiyo juzi saa 2:00 usiku na kwenda kuizika eneo la Marangu Samanga.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Roman Mongi, ambaye ni ndugu wa marehemu Frank Mongi, alisema awali waliukataa mwili huo kwa kuwa ndugu yao alikuwa mwembamba lakini maiti ilionyesha alikuwa mnene.
Alisema walipokuta maiti imewekewa lebo yenye jina la Ibrahim Msuya, waliwasiliana na ndugu wa marehemu huyo waliokuwa wilayani Mwanga.
“Walitutaka tuupige picha huo mwili uliokuwa na jina la Ibrahim Msuya, halafu tuwatumie picha kwa WhatsApp. Ndipo wakasema hakuwa ndugu yao na kwamba waliouchukua ndiyo wa kwao,” alisema.