Wizara Zahamia Dodoma Asilimia 100...!!!


AZMA ya serikali ya kuhamia Dodoma imetimia kwa asilimia 100 kutokana na wizara takribani zote kuhamia mjini Dodoma. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi ametoa kauli hiyo jana mjini Dodoma wakati akizungumza na Kamati Maalumu ya Makatibu Wakuu ambao kwa mara ya kwanza wamefanya vikao vyao mjini hapa tangu serikali ilipofanya uamuzi wa kuhamia hapa.

“Mkutano wa Kamati Maalumu wa Makatibu Wakuu wa wizara zote ni kielelezo dhahiri cha utekelezaji wa azma ya serikali kuhamia Dodoma,” ameeleza. Balozi Kijazi ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Mawaziri, alisema hadi kufikia Machi mosi mwaka huu, takribani wizara zote zimehamia Dodoma, utaratibu huo ambao ulizinduliwa rasmi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Septemba 30, 2016.

Amewashukuru Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, lakini pia alitoa rai kwa wananchi kuzitumia fursa zilizopo mjini hapa za biashara na uwekezaji, huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii pamoja na kujenga Tanzania mpya.

Kuhamia mjini hapa, kunaifanya awamu ya kwanza ya mpango wa Serikali wa kuhamia kwa mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, naibu makatibu na baadhi ya wakurugenzi uwe umetekelezwa kwa ufanisi mkubwa na sasa macho yanaelekezwa katika awamu ya pili.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amesema tayari ofisi yake inapokea taarifa za idadi ya watendaji waliohamia Dodoma.

“Tayari ninapokea taarifa za mawaziri, makatibu na watendaji wa wizara kuhamia Dodoma na naziweka sawa, nitakaa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili kuziweka hadharani,” amesema Jenista, na kuongeza kuwa baada ya kuzihakiki na Waziri Mkuu, ndipo atazungumza na vyombo vya habari kuhusu kuhamia Dodoma.

Amesema kazi ya kukusanya taarifa ikikamilika, serikali itatoa taarifa kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kukamilika kwa awamu ya kwanza Februari 28, mwaka huu, namna lilivyokwenda.

Katika kuhama huko kwa serikali, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimetoa mchango mkubwa wa kuruhusu wizara nane kutumia majengo yake pamoja na Mfuko wa Serikali za Mitaa (LAPF) wizara tatu, na Hazina Ndogo iliyopokea wizara mbili.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad