Yanga imetolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulazimishwa suluhu na Zanaco mjini Lusaka jana.
Suluhu hiyo imeifanya Zanaco kunufaika na bao walilopata katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam wiki iliyopita walipoilazimisha Yanga sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, hivyo bao la ugenini kuwapa faida.
Kwa matokeo hayo, Yanga inashuka katika Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa miongoni mwa timu 16 zitakazotoka Ligi ya Mabingwa Afrika na kucheza mchezo mmoja kabla ya kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo.
Lwandamina afunguka
Kocha wa Yanga, George Lwandamina amesema anapata wakati mgumu katika kazi yake kutokana na kutofanya maandalizi ya mwanzo wa msimu na mabingwa hao wa Tanzania.
Lwandamina alisema hali ya majeruhi inayowaandama wachezaji wake pamoja na kushindwa kubadilika kwa aina ya uchezaji kwa nyota wake vimechangia hali waliyonayo sasa ya kushindwa kuwa na kiwango cha uwiano sawa.
Katika kipindi cha hivi karibuni baadhi ya wachezaji nyota wa Yanga kama Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Thaban Kamusoko wamekuwa wakisumbuliwa na majeraha, jambo ambalo limeipa timu hiyo wakati mgumu.
Kocha huyo aliyejiunga na Yanga mwishoni mwa mwaka jana, alisema kama wachezaji wanapata maandalizi mazuri mwanzoni mwa msimu, wanaweza kucheza msimu mzima kwa kiwango cha juu lakini kama hawakufanya hivyo ni ngumu kuwabadilisha.
“Katika soka hakuna msingi mkubwa kama maandalizi ya mwanzo wa msimu. Wakati huu ndiyo mchezaji anajengewa uwezo wa kucheza kwa kiwango bora kwa msimu mzima,” alisema kocha huyo wa zamani wa Zesco United ya hapa Zambia.
“Mchezaji akifanya mazoezi kwa wiki sita kabla ya msimu kuanza ndipo anaongeza kasi ya mishipa kusambaza damu mwilini. Utimamu wa mwili wake pamoja na uvumilivu mchezo, tofauti na hapo ni ngumu kusonga mbele,” alisema kocha huyo.
Lwandamina alisema kutokana na kubanwa na mechi nyingi za mashindano, ameshindwa kuingiza falsafa yake moja kwa moja klabuni hapo kwani muda mwingi anautumia katika kuangalia wachezaji wanapumzika vipi na wanawezaje kupata utimamu wa kucheza mechi inayofuata.
“Ratiba imebana, kuna wakati ninatamani kuwafundisha vitu vipya lakini hivi navyo vinahitaji muda.
“Tumekuwa na mechi mfululizo msimu huu, mara nyingi ninatazama namna ya kuwasaidia wachezaji kurejesha viwango vyao kwanza.
“Ni vigumu kufundisha katika mazingira hayo hasa unapotaka kuleta vitu vipya. Ni lazima utazame wachezaji ulio nao kama wana uwezo wa kubadilika, vinginevyo inakuwa tatizo,” alisema kocha huyo.
Mchezo ulivyokuwa
Yanga ilishuka uwanjani ikiwa na mabadiliko kadhaa katika kikosi chake tofauti na kile kilichocheza mchezo wa Dar es Salaam. Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alianzia benchi huku Vincent Bossou na Kelvin Yondani kuanza katika nafasi ya ulinzi wa kati.
Kipindi cha kwanza Yanga ilitawala mchezo kwa kiasi kikubwa na mara nyingi ilitengeneza mashambulizi yake kutokea katikati kwa Thaban Kamusoko.
Kurejea kwa Haruna Niyonzima katika kikosi kuliongeza umiliki wa mpira na Zanaco walilazimika kutumia muda mwingi kujilinda na kushambulizi kwa kushtukiza.
Nafasi ya wazi zaidi kwa Yanga katika kipindi cha kwanza ilipatikana dakika ya 30, wakati Kamusoko alipopokea mpira akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini alishindwa kufanya uamuzi na kutoa pasi fyongo.
Mashambulizi mengine makubwa ya Yanga yalitokea dakika ya 14 na 17, kwa Obrey Chirwa na Geofrey Mwashiuya lakini hata hivyo hawakuwa makini na lango.