MKAZI mmoja wa kijiji cha Mwenge kata ya Kate wilayani Nkasi mkoani Rukwa Joseph Songaleli (56) amefariki dunia baada ya kupigwa na watu wasiojulikana akituhumiwa kuwa ni mshirikina.
Akizungumza Mwenyekiti wa kijiji hicho, Medadi Kitinsi, alisema marehemu alivamiwa nyumbani kwake majira ya saa 6:00 usiku na watu wasiojulikana huku wakiwa na silaha za jadi na kuvunja mlango wa nyumba kwa kutumia jiwe kubwa aina ya fatuma na kumshambulia mtu huyo.
Alisema kuwa awali mke wa marehemu baada ya mlango kuvunjwa alikimbia na kutokea dirishani ndipo wauaji hao walipopata nafasi ya kumkamata marehemu na kuanza kumshambulia kwa silaha hizo za jadi.
Alidai kuwa kulitokea mapambano makali kati yao ambapo marehemu alijitahidi kujiokoa lakini alizidiwa nguvu na watu hao walimuamuru marehemu alale kifudifudi na ndipo alipoanza kukatwa mapanga kichwani hadi kufikia kifo chake.
Mwenyekiti huyo wa kijiji amedai kuwa mauaji hayo chanzo chake kikuu ni imani za kishirikina ambapo inasemekana marehemu aliingia mgogoro na mmoja wa ndugu zake akidai kuwa marehemu alikua akimroga.
Habari za Kipolisi zinadai kuwa mpaka sasa wanamshikilia mtu mmoja kuhusika na tukio hilo na kuwa uchunguzi zaidi unaendelea ili kuweza kuwakamata wale wote waliohusika katika tukio hilo.
Mkuu wa wilaya Nkasi Said Mtanda amesikitishwa na mauaji hayo na kuwa serikali inachokifanya ni kuhakikisha wale waliohusika wamnakamatwa na sasa wataanza kupita kila kijiji na kuanza kuielimisha jamii juu ya imani hizo potofu.