OPARESHENI ya kusaka majambazi yaliyoua polisi nane katika eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa wilayani ya Kibiti mkoani Pwani katikati ya wiki iliyopita, ni siri kwa sasa na haitatolewa maelezo kwa vyombo vya habari.
Polisi imesema haiwezi kuweka hadharani operesheni hiyo kwa sasa kwa sababu kufanya hivyo kutaanika kila kitu kinachofanywa na kikosi cha oparesheni katika kuchunguza tukio hilo.
Tukio hilo la kuuawa askari polisi lilitokea Alhamisi saa 12:15 jioni wakati polisi waliotoka lindo wakielekea kambini.
Waliouawa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Peter Kigugu, askari mwenye namba F.3451, Koplo Francis, F.6990 Konstebo Haruna, G. 3247 Konstebo Jacskon, H.1872 Konstebo Zacharia, H.5503 Konstebo Siwale, H. 7629 Konstebo Maswi na H. 7680 Konstebo Ayoub.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Jeshi hilo nchini, IGP Ernest Mangu alisema si kila taarifa ya uchunguzi wa oparesheni hiyo itakuwa ikiwekwa wazi.
Hata hivyo IGP alisema msemaji wa tukio hilo ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba naye alipoulizwa kuhusu maendeleo ya operesheni hiyo, alisema msemaji wa suala hilo ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi alisema oparesheni hiyo bado inaendelea na kwamba ni mpaka baada ya kukamilika ndipo taarifa itatolewa kwa umma.
Alipoulizwa kama kuna watu waliokamatwa au kushikiliwa hadi sasa, alisema siyo kila taarifa ya uchunguzi inafaa kuwekwa hadharani, na kusisitiza kuwa endapo uchunguzi utakamilika taarifa itatolewa.
“Oparesheni inaendelea, kama ikikamilika taarifa itatolewa, lakini kwa sasa hatuwezi kuwa tunasema kila kitu,” alisema.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Ijumaa, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Makao Makuu ya jeshi hilo, Nsato Mssanzya, alisema "vita" dhidi ya majambazi hao ilianza muda mchache baada ya tukio hilo na polisi iliua wahalifu wanne.
Mssanzya alisema polisi iliua majambazi wanne wakati wao wakiua polisi nane.
“Wiki hii ikipita magoli (yetu) yatakuwa mengi kuliko yao (akimaanisha vifo), tutahakikisha kuwa hakuna jambazi atakayesalia popote alipo hata kama amekimbilia kwenye makazi ya watu, tutawasaka,” alisema.
Mssanzya alisema majambazi hao walipora silaha saba ambazo ni SMG nne na Long Range tatu zikiwa na risasi zake.
Alisema baada ya tukio hilo hatua za kiintelejensia zilifanyika ambapo vikosi vya polisi vilivamia kambi ya muda ya majambazi hao na kuwaua wanne lakini wengine ambao idadi yao haikujulikana walitoroka.
Alisema katika kambi hiyo ya muda walipata bunduki nne ambapo mbili ni zile zilizochukuliwa kutoka kwa polisi nane waliouawa.
Mssanzya alisema tukio hilo ni baya na kwamba jeshi la polisi limeshapoteza zaidi ya askari 10 katika matukio kama hayo mwaka huu.
“Kitendo hichi hakikubaliki," alisema Mssanzya. "Nimepoteza askari zaidi ya 10 nina amini wanatosha sasa."
"Kuanzia sasa jeshi la polisi linaenda katika operesheni maalum, hatuna mzaha hatuna msamaha.
“Tutafanya kile jeshi la polisi linatakiwa kufanya tutawafuata popote walipo, tutawashughulikia kikamilifu, nasema hakuna atakayesalia, huu ni mwanzo na hakuna mwisho.
“Wananchi mtuwie radhi, tunawaomba mtuunge mkono katika hili (maana) mtaona sura halisi ya jeshi la polisi, ili tuchukue hatua stahiki, watu wanaotaka kufanya ujambazi watambue dawa ya moto ni moto.”
Alisema operesheni hiyo inayoendelea kwenye mapori hayo na maeneo mengine inahusisha vyombo vya ulinzi na usalama.