Siku chache baada ya kusemekana amepona kutoka kwenye utumiaji uliopitiliza wa madawa ya kulevya ‘unga’ hadi kuwa teja, mkongwe wa Bongo Fleva, Rashidi Makwiro ‘Chid Benz’ sasa inadaiwa kapelekwa kuishi kwa muda Zanzibar ‘Zenji’ baada ya kutoka soba, mkoani Iringa.
MANENO YA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Chid amepelekwa kuishi Zenji ili kumuepusha na kampani za Jiji la Dar es Salaam hususan, maeneo ya Kinondoni ambayo yanadaiwa kuwaharibu mastaa wengi kwa kuingia kwenye madawa, pia kumuondoa kwenye mazingira aliyoyazoea na kwenda ugenini ili kubadili fikra.
BONYEZA HAPA KUSIKIA
“Ni kweli Chid amepelekwa Zenji ili akatulie huko, ndugu na watu wake wa karibu wanahofia kama angebaki Dar basi angeweza kujikuta akirudia tena kubwia unga kama zamani kama wasanii wengine wanaodaiwa kurudia,” kilisema chanzo hicho.
AMANI NA CHID
Lakini wakati hayo yakiwa ni madai tu, juzi, Amani lilimtafuta Chid mwenyewe na kuzungumza naye kwa njia ya simu akisema yupo Visiwani Zanzibar na kwamba, afya yake imeimarika kwa kiwango kikubwa na anatarajia kurudi kwenye gemu hivi karibuni.
“Si kweli kwamba nimehamishiwa Zenji ili nisije nikabwia tena unga, mimi mwenyewe nilishabadilika, sitaki kusikia ishu hizo za unga. Kwa sasa niko Zenji kwenye maisha mengine baada ya kutoka kwenye matibabu Iringa. Namshukuru Mungu afya yangu inaendelea kuimarika kila uchwao.
“Kwa jinsi ninavyoendelea natarajia kurudi kwenye gemu muda si mrefu. Kuna ngoma moja iko tayari kwa prodyuza Lamar ambaye amekuwa akiratibu mambo yangu mengi,” alisema Chid Benz.
AWASHAURI VIJANA, WANAMUZIKI
“Nawashauri vijana na wanamuziki wenzangu ambao katika maisha yao hawajawahi kutumia madawa ya kulevya, wasithubutu kuingia katika matumizi hayo, ni hatari, ni fedheha kwani yanapoteza muelekeo wa maisha na dira ya vijana wengi.
“Watu wajaribu kujifunza kwangu mimi na hata wasanii na watu wengine ambao wametangulia mbele za haki kwa sababu ya utumiaji wa unga,” alisema Chid Benz.
TUJIKUMBUSHE
Huko nyuma, Chid Benz alikuwa hajawahi kunaswa laivu akitumia unga lakini Desemba mwaka jana, makachero wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) wa Kampuni ya Global Publishers walimfungia kazi kwa zaidi ya saa 10 na kumnasa mubashara akiwa anatumia unga kwenye gesti moja Kinondoni.
Siku mbili baada ya habari yake kutoka kwenye gazeti ndugu na hili, Risasi Jumatano, watu wake wa karibu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba akitajwa, walimchukua Chid na kumpeleka Iringa kwenye nyumba ya matibabu kwa watu walioathiriwa na madawa ya kulevya ‘sober house’ ambako alianza tiba.
Mwezi uliopita, yaani Machi, Chid aliripotiwa kuendelea vizuri na kurudishwa jijini Dar ambako ndiko kwenye makazi ya familia yake hadi hivi karibuni iliposemekana amepelekwa Zenji kuishi kwa muda