MBUNGE wa Nzega Mjini, Hussein Bashe(CCM), ameiomba Kamati iliyoundwa na Rais John Magufuli kwa ajili ya kuchunguza makontena ya mchanga katika Bandari ya Dar es Salaam, kurekori kilichomo katika makontena hayo ili yaoneshwe kwenye televisheni kwa lengo la kuwaondoa hofu Watanzania.
Ombi hilo limekuja siku chache baada ya Rais Magufuli kuunda Kamati kwa ajili ya kuchunguza makontena ya mchanga katika Bandari ya Dar es Salaam.
Alitoa ombi hilo bungeni mjini hapa wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi yaWaziri Mkuu kwa mwaka 2017/2018.
Alisema wengi wanaamini kwamba yale makontena yaliyokamatwa bandarini yana dhahabu.
“Spika kule kwangu Nzega wanaamini yale makontena yaliyopo bandarini yana dhahabu,tunaomba mrekodi hili tukio la uchunguzi halafu mtuoneshe kwenye TV tuone kilichomo ndani ya zile kontena,” alisema.
Alisema yeye ni miongoni mwa watu ambao wanaamini kwamba uwekezaji wa migodi mikubwa haujasaidia nchi ya Tanzania.
“Mimi ni miongoni mwa watu tunaoamini kwamba uwekezaji wa migodi mikubwa hauijaisaidia nchi yetu,”alisema.
Mbunge wa Gairo, Mohamed Shabiby (CCM), amepongeza hatua ya serikali kupiga marufuku matumizi na biashara ya pombe maarufu kama viroba ambapo alisema kuwa hivi sasa watu wamenenepa kutokana na kuacha kutumia kinywaji hicho.
Aliishauri pia serikali kutafuta namna bora ya kuzuia uwepo wa kinywaji hicho akitaka waanzie kwenye uzalishaji badala ya sokoni kama ambavyo wamefanya wakati wa kutekeleza zoezi hilo hivi karibuni nchini.