BEKI wa Yanga, Vincent Bossou, amesema mshambuliaji wa zamani wa Azam, Kipre Tchetche, ni muhimu katika kikosi hicho.
Tchetche ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu Al-Nahda-Buraimi ya Oman, ametajwa ni mshambuliaji pekee anayeweza kuisaidia Yanga.
Akizungumza jana, Bossou alisema Tchetche ni kati ya washambuliaji wa Ligi Kuu Bara waliokuwa wanampa shida ukilinganisha na wengine.
Bossou alisema pamoja na Yanga kuwa na washambuliaji mahiri, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Amis Tambwe, lakini Kipre ana nafasi yake.
Alisema katika misimu miwili aliocheza soka hapa nchini, amekutana na washambuliaji wengi lakini Kipre ni chaguo lake la kwanza.
Bossou alisema angefurahi kama Yanga wangemsajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, kwani ana uwezo mkubwa wa kupiga soka.
“Nimekabana na mastraika wengi hapa Bongo, lakini naweza kusema sijaona straika mzawa au wa kigeni mwenye uwezo kama wa Kipre Tchetche, kocha wetu George Lwandamina anamfahamu vizuri tu jinsi anavyokipiga uwanjani,” alisema Bossou.
Alisema mshambuliaji huyo ni msumbufu kwa mabeki kwani ni mwepesi kwa kupiga chenga na kufunga mabao.
Yanga waliwahi kufukuzia saini ya Tchetche, lakini walishindwa kumsajili na baadaye kutimkia katika klabu hiyo ya Oman.