Chadema Wafichua Haya Mazito Kuhusu Njama za Serikali Kuhusu Zanzibar..!!!


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeihusisha serikali katika mgogoro unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF).

Kwa mujibu wa Chadema, mgogoro huo ndani ya CUF, lengo ni serikali kudhoofisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili kuvigawa vyama vinavyoiunda.

Akizungumza katika kikao maalumu cha Baraza la Uongozi la Chama hicho Kanda ya Kaskazini kilichokutana kwa siku mbili jijini hapa, Naibu

Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika, alidai mgogoro wa CUF una mkono wa serikali, ingawa hakuthibitisha jinsi gani serikali inahusika.

Mnyika ambaye pia alimwakilisha Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Vincent Mashinji, alidai
mgogoro huo una maslahi ya serikali na kwamba umepandikizwa kwa lengo la kuvuruga chama hicho na kudhoofisha harakati za Ukawa.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alidai serikali na CCM wametishwa na nguvu, mipango na harakati za Ukawa vilivyoonekana wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kwamba hali hiyo ndiyo inayowatisha, hivyo kutafuta mbinu za kudhoofisha.

“Mgogoro wa CUF unadhoofisha harakati za Ukawa za kuhakikisha jitihada za kuleta mabadiliko na maendeleo zinafikia malengo, pamoja na hayo hatutatikisika….ndiyo tunaimarika zaidi,” alisema
Mnyika.

Alisema Chadema inaendelea kumtambua Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, na kuwa watashirikiana naye katika harakati za Ukawa na hawamtambui Magdalena Sakaya, aliyetangazwa na Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

MAFANIKIO YA UKAWA

Mnyika alisema Ukawa ilipata mafanikio makubwa kwenye uchaguzi wa 2015 kwa kuibuka na ushindi katika majimbo 22 ya ubunge na kunyakua halmashauri 11 na kutamba kuwa matokeo hayo yanaashiria hatari kwa CCM na serikali yake kung’oka madarakani mwaka 2020.

Naye Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, aliwataka viongozi wa Kanda kuonyesha mfano wa kuongoza kwa kuwapatia wananchi katika majimbo na halmashauri huduma ambazo hawajawahi kuzipata walipokuwa wakiongozwa na CCM kwa miaka mingi.

Aidha, aliwataka viongozi kuwa kimbilio la wanyonge kwa kukubali kujitosa katika masuala muhimu ya kijamii kwa gharama yoyote ili kujenga imani na matumaini kwa Watanzania.

MBOWE AMSIHI MAGUFULI

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alimsihi Rais Magufuli kwa kumtaka asipuuze hoja wanazozitoa wao kama viongozi na kwamba hazina lengo la kumjaribu wala kukosoa utawala wake.

Alisema wanachompa ni ushauri kuhakikisha nchi inasonga mbele kimaendeleo.

“Hakuna chama wala mtu mwenye lengo la kumjaribu rais kwani ana mamlaka makubwa ndani ya nchi hii.

Rais anastahili kupokea na kusikiliza ushauri anaopewa na vyama vya upinzani au taasisi za kijamii zilizoko kwani zinatumika kwa ajili ya kuwakilisha kilio cha wananchi walio wengi ambao wanakosa fursa ya kuwasilisha kero zao,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Naomba Rais Magufuli atambue kwamba hatuna nia ya kumjaribu bali tunamtegemea aongoze nchi hii katika misingi ya kikatiba na kisheria.”

KUHUSU BAJETI

Kwa upande wa bajeti ya 2017/18, aliitaka serikali kuhakikisha inakuja na mpango wa maendeleo ambao unatekelezeka badala ya kukopa fedha kutoka kwa wahisani kwa ajili ya kujiendesha huku miradi ya kimaendeleo ikishindwa kutekelezwa.

Alisema kuendelea kukopa kunasababisha deni la taifa kuongezeka kila uchao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad