Wapinzani wawili katika mgogoro wa uongozi wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Profesa Ibrahim Lipumba sasa wamefikia pabaya baada ya kuamua kupambana kuichukua ofisi ya makao makuu iliyopo Buguruni.
Kwa sasa ofisi hiyo inatumiwa na Profesa Lipumba, ambaye uamuzi wake wa kurejea madarakani mwaka mmoja baada ya kujiuzulu uenyekiti na nyadhifa nyingine zote, unapingwa na kundi lililopanga kuzichukua ofisi hizo Jumapili.
Jana, kundi linalompinga Profesa Lipumba lilitangaza kuwa litakwenda ofisi hizo Jumapili kwa ajili ya kusafisha “kila kitu ambacho hakitakiwi kiwepo”, lakini mwenyekiti huyo amesema ameshajiandaa kukabiliana nao na ameripoti suala hilo polisi.
Profesa Lipumba alisema hayo jana, ikiwa ni siku moja tangu Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limtake ajitokeze kuzungumzia kitendo cha walinzi wa CUF kuwashambulia waandishi wa habari waliokuwa kwenye mkutano ulioandaliwa na viongozi wa chama hicho Kinondoni.
Profesa Lipumba alikuwa akiwajibu wabunge wa CUF wanaomuunga mkono Maalim Seif waliowaambia wanahabari katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana kuwa wamepanga kwenda ofisi za Buguruni Jumapili ijayo na wataungana na wanachama wengine kufanya usafi.
“Tulianza kufanya usafi soko la Buguruni, tukamalizia katika ofisi yetu. Kwa hiyo katika hali nzuri, hatuhitaji wabunge wasumbuke kufanya usafi siku hiyo,” alisema Profesa Lipumba
Profesa Lipumba alisema watu hao hawana nia ya dhati ya kufanya usafi, bali wamepanga kufanya vurugu katika ofisi hizo kwa kushirikiana na watu wa chama kingine cha upinzani.
“Wanataka kuleta vurugu ili CUF ionekane na taswira mbaya kwa Watanzania. Naomba wanachama waepuke mtego huu, namshauri (Mbunge wa Temeke, Abdallah) Mtolea akafanye usafi huo Temeke mbona kuna masoko mengi tu machafu?” alisema.
Awali mjini Dodoma, wabunge wanaomuunga Maalim Seif walisema watakwenda na vifaa vya usafikuondoa kila uchafu watakaoukuta
“Wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) ambao hawamkubali Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti, wameamua kwenda kufanya usafi kwenye ofisi zao za Buguruni, ofisi kuu ya CUF Buguruni,” alisema Mtolea akiwa ameambatana na wabunge wenzake katika mkutano na waandishi uliofanyika chumba cha habari cha Bunge.
“Na hatua hii imekuja baada ya kuona ofisi ile inatumika vibaya. Imekuwa ndio kijiwe cha wahuni kupanga matukio ya kihalifu. Kwenda kuvamia mikutano, kwenda kuwavamia watu na kadhalika. Sasa sisi kama wanachama tumeona hatuwezi kuiacha hali hiyo iendelee.”
Aliwataka wanachama kutoka maeneo ya Dar es Salaam, Pwani na mikoa mingine wafike kufanya usafi huo.
Alipoulizwa aina ya uchafu wanaoenda kuuondoa, Mtolea alijibu “ni kitu chochote ambacho hakiko mahali pake” na kwamba hata Profesa Lipumba hayuko mahali pake.
“Tangu Msajili amtambue Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti, hatujawahi kwenda katika ofisi yetu ya Buguruni, matokeo yake ofisi hiyo imekuwa na uchafu mwingi na kuwa pango la wahuni,” alisema Mtolea.
Alipoulizwa uwezekano wa kutokea vurugu, Mtolea alisema hawajiandai kufanya fujo, bali kufanya usafi.
Kuhusu kesi iliyopo mahakamani kuhusu mgogoro huo, alisema ile inapinga msajili kumtambua Lipumba na haizuii kusafisha ofisi yao.
Alisema hawaendi kuteka ofisi hizo, bali wanakwenda kwenye ofisi zao hivyo hawahitaji kuomba ruhusa kwa mtu yeyote.
“Ofisi ni chafu, sisi tunataka tukaisafishe kwa sababu imekuwa sehemu ya kupanga mipango mibaya kwa mustakabali wa chama,” alisema.
Akiweka msisitizo wa jibu hilo, Mbunge wa Chambani, Yusuf Salim Hussein alisema hakuna silaha ya moto inayoshinda nguvu ya umma.
Awali, wabunge hao walitoa tamko la kuunga mkono tamko la TEF kuhusu kulaani kitendo cha wafuasi wa Profesa Lipumba kuwashambulia waandishi wa habari.
Mnadhimu wa chama hicho na Mbunge wa Malindi, Ally Salehe alisema TEF imetoa tamko zito la kutaka waandishi wa habari kufanya kazi kwa usalama na uhuru.
“Na isiwe TEF tu, tunataka watu wote waliokerwa na tukio hilo watoe tamko la kulaani,” alisema.
Kuhusu tamko la TEF, Profesa Lipumba alisema atatoa tamko kuhusu suala hilo ifikapo leo.
“Mimi ni muumini wa demokrasia. Hapa ninavyoongea na wewe nipo katika hatua ya mwisho ya kumalizia kuandika barua kuelekea TEF ambayo itafika kati ya leo (jana) jioni au kesho,” alisema.
Hata hivyo, alisema mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano kwa umma, Abdul Kambaya alitoa tamko kuhusu tukio hilo.
Katika tamko lake, Kambaya alisema mmoja wa watu walioshiriki kushambulia mkutano ni mlinzi wao na kwamba alikuwa katika doria kudhibiti wanachama wanaofanya mikutano hotelini.