Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano wa CUF –Maalim, Salim Bimani ameshangazwa na kauli ya wafuasi wa CUF-Lipumba kuwa waliovamia mkutano wa Vina wiki iliyopita ni walinzi wa chama hicho waliokuwa doria.
Pia Bimani amewahoji CUF –Lipumba maswali mawili. La kwanza ni kwa nini wafanye doria ghorofa ya nne wakati wao sio askari? Swali jingine alilolihoji Bimani ni kwa nini walikuja na bastola?
Jana, Mkurugenzi wa Habari wa CUF-Lipumba, Maulid Kambaya alisema aliyekatwa kisigino ni mlinzi wa chama aliyekwenda kufanya doria na kuwa hakupigwa na wananchi bali wafuasi wa CUF-Maalim.
Lakini Bimani alisema:
“Umesema Kambaya anasema walikuwa katika doria? Mngemuuliza doria gani inafanyika floor ya nne wakati wao siyo askari huu ni uongo wa mchana kweupe,”alisema Bimani.
Alisisitiza kuwa upande wa Profesa Lipumba ndiyo unao husika na tukio hilo, kwani siyo mara kwanza kutuma kundi kama hilo kufanya vurugu wakiwa na silaha mbalimbali
Kwa mujibu wa Bimani, kundi hilo lilishafanya vurugu katika mahakama kuu hivyo hakuna cha kujitetea badala yake mamlaka husika ziwachukulie hatua kwa kitendo hicho.
“Yule kijana aliyejeruhiwa na wananchi ambao walimdhibiti, siyo upande wa Maalim kama anayodai Kambaya.Hivi Kambaya kusoma hajui hata picha haoni kujua nani aliyehusika,”alihoji Bimani.