VIONGOZI na wanachama wa CUF wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa chama hicho (JUKECUF), Fatma Fereji wamesema wapo tayari kukabiliana na njama ovu dhidi ya chama hicho na kwamba watakilinda kwa gharama zozote zile.
Wanachama hao waliyasema hayo wakati wa ziara ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alikuwa katika ziara ya siku 10 katika kisiwa cha Unguja.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi Habari Uenezi na Mahusiano, Mbarala Maharagande ilibainisha kuwa uamuzi huo umetolewa na wana CUF ikiwa ni kutambua mchango wa katibu mkuu wao katika kujenga chama.
Alisema katibu mkuu huyo amekuwa akifanya ziara katika Kisiwa cha Unguja kuanzia Aprili mosi mwaka huu ziara ambayo imekuwa na mafanikio makubwa.
Maharagande alisema wazo hilo la kujitolea kulinda chama lilitolewa na wanachama wakati Maalim Seif akifanya kikao cha majumuisho na tathmini katika ofisi ya CUF iliyoko Kilimahewa Wilaya ya Mjini-Unguja.
“Ziara hiyo imepata mafanikio makubwa na kufikia malengo yaliyowekwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF. Miongoni mwa kazi alizofanya katika ziara hiyo ni pamoja na kukabidhi majukumu kwa waratibu wa chama, ambapo jumla ya waratibu 4,727 walipatikana na ndipo uamuzi wa kukitolea ulitokea,” alisema.
Aidha, alisema katika ziara hiyo Maalim Seif aliweka mawe ya msingi katika maeneo sita, Baraza 14, majengo sita, na kukabidhiwa viwanja viwili kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Chama.
Naibu mkurugenzi huyo alisema ziara hiyo ilifanikisha kupatikana wanachama wapya 591 kati yao wanachama 124 walitoka CCM.
Alisema katika kuhitimisha ziara hiyo, chama kiliwapatia nishani maalum wanawake saba walio mstari wa mbele katika kutumia rasilimali zao kwa ajili ya chama.
Katika hatua nyingine, Mahagande alisema wabunge wa CUF wameendelea na ziara za kuimarisha chama katika wilaya mbalimbali ikiwa ni sehemu ya utaratibu waliojiwekea kila wiki wakiwa bungeni Dodoma.
Aliwataja baadhi ya wabunge ambao walifanya ziara katika Wilaya ya Kondoa kuwa ni Masoud Abdallah Salim (Mtambile), Saumu Sakala (Viti Maalum), Twahir Awezu Mohamed (Mkoani), Juma Kombo Hamad (Wingwi), Mbarouk Salim Ali (Wete) na Mussa Mbarouk (Tanga).
Alisema wabunge hao wakiwa Kondoa walikutana na kufanya vikao na viongozi wa kata, wajumbe wa kamati ya utendaji wilaya pamoja na madiwani wa CUF na kuweka ratiba ya kuwafikia wanachama wengi zaidi.
Alisema wilaya na mikoani itakayofikiwa hivi karibuni ni pamoja na Morogoro Mjini, Tanga, Pangani, Shinyanga, Nyamagana, Ilemela-Mwanza, Lindi na Tabora.
Halikadhalika Mahagande alisema shauri la msingi namba 23/2016 lililopo kwa Jaji Kihiyo dhidi ya Msajili Jaji Francis Mutungi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake limepangwa kutajwa tena Aprili 24 mwaka huu.
Aidha, alisema shauri la wizi wa fedha za ruzuku limepangwa kusikilizwa Aprili 20 mwaka huu kuhusu zuio la Lipumba na wenzake kupewa fedha za ruzuku na Aprili 24 mwaka huu shauri la msingi mbele ya Jaji Dyansobera.