CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema Msajili wa Vyama Vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ndiye chanzo cha yanayoendelea ndani yake kwa kuasisi makundi maovu.
CUF imedai Msajili huyo ni chanzo cha makundi ya mazombi, Mungiki, wavamizi, wabeba bastola na mapanga yaliyoshiriki matukio ya utekaji wanachama, viongozi wao, hata watu wa chama hicho kupigwa visu mahakamani.
Hata hivyo, alipotafutwa Msajili kuzungumzia tuhuma hizo hakupatikana, lakini Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Monica Laurent alisema ofisi yake haiwezi kusema lolote, kwani anachojua suala la CUF liko mahakamani na kinachosubiriwa ni Mahakama kutenda haki.
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa chama hicho upande wa Maalim Seif Sharif Hamad, Salim Bimani alimtaja Jaji Mutungi kuwa aliyesababisha pia mlezi wa vitendo hivyo vya kihalifu ikiwamo kuvamiwa kwa Ofisi Kuu ya Chama ya Buguruni Dar es Salaam Septemba 24 mwaka jana.
“CUF haikubaliani na inalaani tamko la kinafiki la Jaji Mutungi na tunamtaka avunje ushirikiano hasi wa kuhujumu chama alioujenga kati yake, Profesa Ibrahim Lipumba na Jeshi la Polisi,” alidai Bimani.
Alitaja orodha ya matukio na dosari katika tamko la Jaji Mutungi, akisema kiongozi huyo alifanya makusudi ili kuchochea vurugu ndani ya CUF kwa kilichodaiwa kuwa ni kwa maslahi binafsi au waliomtuma.
Alisema Jaji Mutungi amekuwa mfuasi wa Profesa Lipumba na mkereketwa kuliko wana CUF wenyewe na kwamba, wakati timu ya Profesa Lipumba inakiri kuwa Juma Mkumbi ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Kinondoni na Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Mutungi hajui na hataki kukubali.
Aliongeza kuwa Jaji Mutungi alimwandikia Mkuu wa Polisi–IGP, ampe ushirikiano wa kila hali Lipumba kila unapohitajika na asikilizwe kwa kila anacholielekeza Jeshi hilo, akidai kuwa ushahidi wa yanayoendelea hauhitaji tochi.
Alitaja matukio mengine kuwa ni pamoja na Jaji Mutungi kufanikisha wizi wa fedha za ruzuku Sh milioni 369 na kwamba hilo lilifanyika huku Mutungi akijua mwajibikaji katika masuala ya fedha ni Katibu Mkuu.
Bimani alimshutumu pia Jaji Mutungi kuwa alipanga na Profesa Lipumba kuundwa Baraza Kuu bandia kisha kuteua Bodi bandia ya Wadhamini baada ya kuona kesi imewakalia vibaya mahakamani.
Alidai kuwa kutokana na hali hiyo, kwa mtazamo wao Jaji Mutungi amepoteza hadhi ya kuwa Jaji na anaivunjia heshima nafasi hiyo, kwani amepoteza uadilifu na kamwe CUF haitakubaliana na uovu aliouasisi na kuusimamia.
Alisisitiza kuwa CUF haitakubaliana na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa chochote kitakachokuwa kinyume na matakwa ya sheria.
Aliongeza kuwa CUF ni taasisi imara ya kisiasa nchini yenye viongozi makini, itakayoendelea kujenga uhusiano na ushirikiano mwema na wadau wenye dhamira ya dhati ya kustawisha na kuchochea misingi ya demokrasia ya kweli nchini, utawala wa sheria, kulinda na kutetea haki za binadamu, amani na kuunganisha Watanzania wote.