FAHAMU Mambo Muhimu Yanayokupasa Kuzingatia Ukiwa Kama Kijana..!!!


Matatizo mengi yanayowatokea binadamu husababishwa na mwanzo mbaya wa mipango ya maisha yake. Ni asilimia ndogo sana ya matatizo hutokea kwa bahati mbaya tu kutokana na sababu za hapa na pale.

Lakini mengi kati yao, husababishwa na kwenda ilimradi siku zinakwenda. Wale wanaopanga mambo yao mapema huwa hawana kitu kigeni kwenye maisha yao. Kila kitu kinachotokea huwa kwa sababu tayari walishajipanga kabla hakijatokea.

Binadamu makini mwenye mafaikio na afya njema, pamoja na mabo mengine husababishwa na umakini wake katika hatua na mapito ya maisha yake. Ukiweza hayo, maisha yako yatakuwa rahisi.
Hata hivyo kwa bahati mbaya au kwa kutokujua, wapo ambao hukosea sehemu za hatua za maisha jambo linalosababisha baadae waharibu kabisa maisha yao.

Kama kijana unapaswa kujua mambo muhimu zaidi ambayo unapaswa kuyafanya ili maisha yako yawe bora. Kwa hakika mambo haya , kama yakizingatiwa bila shaka kijana atakuwa amejenga msingi imara wa maisha yake na kwamba huko mbele atakuwa mjuzi wa mambo mengi, akiwa na maarifa chanya yatakayomjenga kimaisha.

Imarisha imani yako katika dini

Hofu ya Mungu ni kitu cha muhimu sana katika maisha. Lakini huwezi kuwa na hofu kama ukiwa huna imani. Inawezekana unayo imani yako kiasili, lakini usiwe mshirika mkamilifu wa imani hiyo, 
katika maisha ni kosa. Kuijua, kujifunza, kuifuata, kuitii na kuipenda imani yako itakusaidia sana maishani. Mtu mwenye kuifuata imani yake, bila shaka atakuwa mbali na vitu vibaya.

Ukimjua Mungu hutaiba, hutasema uongo, hutadhulumu wala kufanya mambo mengine yanayofanana na hayo ambayo kimsingi si ya kuwapendeza hata binadamu wenzako.

Msingi wa yote hayo ni kwamba utakuwa kioo kwenye maisha na hapo utapata marafiki wengi watakaokusaidia kutimiza ndoto za maisha yako.

Utii kwa wazazi

Hili ni jambo la msingi sana, uzuri ni kwamba jambo hili limeelekezwa hadi katika vitabu vya dini. Kwamba watoto wana wajibu wa kuwaheshimu na kuwapenda wazazi wao.Heshima kwa mzazi kuna faida nyingi, utakuwa na hakika ya kupata radhi zao, hivyo kuwa na uhakika wa kuishi maisha bora.
Kufungamana na jamii

Mafanikio ya maisha yana uhusiano mkubwa sana na namna unavyoishi na jamii inayokuzunguka. Ikiwa utaishi kipeke yako kwa kila kitu, jamii itakutenga. Mazoea haya huanzia katika kipindi cha ujana. Lazima kijana atengeneze wigo mpana wa kuwa mshirika mkubwa kwenye mambo mbalimbali ya kijamii.

Kufanya hivyo kutakusaidia sana kusaidika pale unapokuwa na matatizo. Shiriki kwenye shughuli za kijamii, mfano msiba, sherehe nk. Kujichanganya kwako kutakuweka karibu zaidi na jamii 
inayokuzunguka. Muhimu zaidi ni kwamba, utakuwa sehemu ya jamii na siku zote tunasema mtaji namba moja kwenye maisha ni watu. Ukiwa na watu hesabu maisha yako ni rahisi. Ni kweli vitu muhimu ni fedha, wazo na watu, lakini cha kwanza kati ya vyote ni watu.

Acha tabia ya  kupoteza muda wako sana.

Kuna wakati unaweza usifanikiwe sio kwa sababu huna malengo na mipango mizuri uliyojiwekea ila ni kwa sababu unapoteza muda mwingi katika mambo yasiyo ya msingi na  ya lazima katika upande wa maisha yetu. Na hili ndilo moja ya kosa kubwa wanalofanya vijana na linawazuia kufanikiwa.

Ni ukweli uliowazi ukiwa kijana umekuwa ukipoteza muda mwingi sana kwenye mitandao ya kijamii ambapo ukiangalia kwa makini hakuna unachokifanya huko kikubwa zaidi ya kupoteza muda wako wa thamani ambapo pengine ungeweza kuutumia kukuzalishia.

Kama unataka kugeuza maisha yako na kuwa ya mafanikio zaidi acha kuchezea muda wako kama unavyofanya sasa. Acha kujivunia ujana ulionao kwa kuamini unao muda wa kutosha. Mapinduzi makubwa juu ya maisha yako unatakiwa uyafanye ukiwa bado kijana. Sasa huwezi kuleta mabadiliko kama utakuwa ni mtu wa kupoteza muda sana. Pangilia muda wako vizuri kisha fuata malengo yako.

Acha kuishi na watu wasio sahihi kwako.

Maisha yako kwa sehemu kubwa umekuwa ukiyafanya kuwa magumu kutokana na kushikilia marafiki wengi ambao sio msaada kwako. Hebu jaribu kuchunguza wewe mwenyewe marafiki ulionao wanakusaidia vipi kukufikisha kule unakotaka kufika katika maisha yako.

Utakuja kugundua kuwa marafiki wengi ulionao ni walewale ambao hawana msaada sana kwako zaidi ya kukurudisha nyuma kimafanikio. Ukiwa katika hali hii upo kwenye hatari kubwa sana, kwani mara nyingi marafiki zako wana nguvu kubwa sana ya kubadili maisha yako kuliko unavyofikiri.

Ili kuweza kubadilisha maisha yako ni lazima kwako kubadili mwelekeo haraka sana na kuchagua marafiki watakaoweza kukusaidia kufanikisha malengo yako kwa sehemu kubwa. Ukiweza kufanya hivyo utakuwa umejiweka kwenye nafasi kubwa sana ya kuweza kufanikiwa.

Usiogope kuchekwa kwa kile unachotaka kufanya.

Mara nyingi umekuwa na fikra za kuogopa kuchekwa kila unapojifikiria kufanya kazi ya aina fulani. Na hili linasababishwa hasa kila unapoangalia elimu uliyonayo unakuwa unajihisi huwezi kufanya kazi fulani kwa sababu ni ya watu wa chini sana katika maisha.

Kwa kuhofia kwako kuchekwa hivyo ndivyo ambavyo umekuwa ukizidi kujichelewesha kufikia malengo yako. Kumbuka kazi ni kazi, kama utaendelea kuogopa watu katika maisha yako kuwa watakucheka kwa jambo unalotaka kulifanya utakuwa unajichelewesha mwenyewe kufanikiwa.

Tambua maisha yako ni maisha yako wewe, usimuogope mtu na kuhisi kuwa atakucheka eti kwa sababu unafanya kitu fulani. Hata ikitokea wamekucheka hiyo  haitasaidia kitu endelea na maisha yako. Kuwa na fikra chanya, achana na mawazo potofu ya vijana wenzako ya kuamini kuchekwa. Ukiendekeza ugonjwa huu wa kuogopa kuchekwa, hakika huwezi kufanikiwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad