Mbunge wa jimbo la Kawe kwa tiketi ya CHADEMA Mhe. Halima Mdee jana amefunguka na kuomba radhi bungeni kufuatia kutoa lugha isiyokuwa na staha bungeni wakati wa uchaguzi wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki uliofanyika April 4, 2017.
Halima Mdee wakati akiomba radhi hiyo anasema kuwa siku hiyo ya uchaguzi kulikuwa na matukio ambayo yalikuwa yakiendelea bungeni ambayo yalimpelekea kutoa lugha isiyokuwa sawa kitamaduni za bunge, ambayo ilimgusa Spika wa Bunge na Naibu waziri wa Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Khamis Kigwangala "Mhe. Mwenyekiti tarehe 4 mwezi wa 4 wakati wa uchaguzi wa EALA kuna matukio ambayo yalikuwa yanaendelea yakanipelekea kuzungumza lugha ambayo kitamaduni za Bunge si sawa na lugha husika ilimgusa Spika wa bunge na Mhe, Kigwangala kwa namna moja au nyingine kama mbunge mzoefu nilitumia jitihada binafsi kuzungumza na kuomba radhi wahusika katika 'individual capacity'lakini vilevile nikaona ni busara kwa sababu haya maneno niliyasema bungeni hivyo kuzungumza pia hapa na kumuomba radhi Mhe. Spika kwa hiyo niliomba huu muda kwa lengo la kumuomba radhi, kumwambia namuheshimu na kumwambia sitarudia" alisema Halima Mdee
Mbali na hilo Halima Mdee aliendelea kuomba radhi kwa wabunge, watanzania pamoja na wananchi wa jimbo la Kawe lakini pia Halima Mdee alisisitiza kuwa michango yake ya bunge itaendelea kama kawaida yake lakini kwa kutumia lugha za staa.