MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, ametangaza kuanza kwa kampeni ya kumsaka Ben Saanane, ambaye ni msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, aliyepotea tangu Novemba mwaka jana.
Mbali na Lema, wanasiasa wengine waliotajwa kuanza kampeni hiyo ya kumsaka Saanane akiwa hai au amekufa, ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo).
Lema alizungumza hayo mjini hapa jana, ikiwa ni siku moja tangu kupatikana kwa msanii Ibrahimu Mussa, maarufu Roma Mkatoliki, aliyetekwa katika mazingira ya kutatanisha Aprili 5, mwaka huu kabla ya kupatikana juzi huku akimtaja kiongozi mmoja wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhusika na vitendo hivyo vya utekaji.
Akifafanua madai hayo, Lema alisema katika mazingira ya kawaida haiwezekani kiongozi huyo autangazie umma kwamba Roma angepatikana kabla ya Jumapili na kweli ikawa hivyo.
Alisema kuwa kutokana na kauli hiyo, ni dhahiri kiongozi huyo alikuwa anajua alipo Roma, huku akifananisha tukio hilo na la Ben.
Alisema timu hiyo ya wabunge inaungana kumtaka kiongozi huyo aeleze alipo Ben kwa sababu watu wanaandamana katika mioyo yao huku wakiwa na uchungu na hasira.
“Unakwenda mwezi wa sita Ben Saanane amepotea, siyo chama wala wazazi, ndugu zake wanaojua alipo, suala la kupotea kwake ni suala la kila binadamu mwenye akili timamu, tulitilie mkazo wote na mimi naamini watawala wanajua mahali alipo Ben,” alisema na kuongeza.
“Kama ambavyo kiongozi wa Dar es Salaam alikuwa anajua mahali alipo Roma na wenzake, Kamanda Sirro hawezi kusema alipo Saanane, ila huyo ndiye anaweza kama alivyosema Roma atapatikana lini, tunamtaka Saanane kama amekufa tupeni mifupa yake tukaizike kwa heshima, kama yu hai mleteni akaungane na ndugu zake na akawe huru katika taifa lililopata uhuru tangu 1961.
“Nitahamasisha vijana nchi nzima kuanzia kwenye mitandao tudai haki ya Saanane kwa nguvu zote na viongozi wa dini watusaidie suala hili kwani wakati Kamanda Sirro anasema Roma hashikiliwi katika kituo chochote cha polisi, kiongozi mmoja alisema Roma na wenzake watapatikana kabla ya Jumapili,”
Lema alisema kuwa Jeshi la Polisi ndio wanahusika na masuala ya upelelezi na siyo ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kudai kushangazwa na hatua ya mkuu huyo kujihusisha katika suala hilo.
“Ni nani amempa mamlaka kuwa msemaji wa masuala ya polisi kwenye masuala yanayohusu raia na mali zao? Kwanini Ben alipopotea hakuna tamko lolote limeshawahi kutolewa na kiongozi huyo au mwingine yeyote?
“Ukisoma kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, mkuu huyo anahusishwa na kupotea kwa Ben, hajawahi kuita vyombo vya habari kukanusha au kusema atamtafuta, kwa sasa taifa linavyoonekana Waziri wa Mambo ya Ndani hapa nchini ni kiongozi huyo,” alisema.
Lema alidai kwa sasa Waziri wa Mambo ya Ndani nchini ni yeye kwa kuwa waziri mwenye dhamana hiyo, Mwigulu Nchemba ameshindwa kutekeleza majukumu yake au anaogopa kuyatekeleza kwa kuhofia kutenguliwa kwenye nafasi hiyo kama ilivyotokea kwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
“Inaonekana kama Mwigulu kazi hii ameishindwa au anaogopa akiyaingilia yatampata yaliyompata Nape, siyo Mwigulu peke yake, mawaziri wengi wamekosa ujasiri wa kusema mambo kadhaa yanayohusu nchi, kwani hata juzi niliongea na Mwigulu akasema hana taarifa wakati yeye anahusika na usalama wa raia,” alisema Lema.
Alitolea mfano nchi ya Tunisia kuwa machafuko yalisababishwa na mmachinga mmoja kujilipua moto na kuwa suala la Ben likiendelea linaweza kukuza hasira na watawala wakifikiri bunduki, vifaru na polisi wanaweza kuzuia hasira za wananchi na kuwa taifa lenye watu
wasio na uhakika wa kuishi, siyo kweli.
“Mimi mwenyewe sina uhakika wa kuishi, ninatembea sijui kama nitatekwa au sitatekwa kwa sababu mpiga kelele yeyote wa masilahi ya taifa hili anaonekana ni kikwazo yuko katika mkakati wa kutekwa,” alisema Lema.